WANAFUNZI 10 KUNUFAIKA NA SAMIA SCHOLARSHIP EXTENDED, KWENDA KUSOMA URUSI


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza fursa mpya ya ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 10 wa Kitanzania kwenda kusoma nchini Urusi kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Agosti 13, 2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema wanafunzi hao wamepata fursa hiyo kutoka Chuo Kikuu cha RUDN cha jijini Moscow, kufuatia ziara rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchini Urusi iliyofanyika Juni mwaka huu.


Profesa Mkenda amesema wanafunzi hao wanatarajiwa kuondoka nchini Septemba 1, 2026, kuelekea Moscow, ambapo wataanza kambi maalumu ya maandalizi ya masomo (bootcamp) itakayodumu kwa takribani miezi 10 kabla ya kuanza masomo yao ya shahada ya kwanza.


“Katika kipindi cha bootcamp, Serikali ya Urusi itagharamia asilimia 80 ya gharama na Samia Scholarship Extended itagharamia asilimia 20,” amesema Profesa Mkenda.


Ameongeza kuwa baada ya wanafunzi hao kukamilisha kambi hiyo na kuanza masomo rasmi ya shahada ya kwanza, Serikali ya Urusi itagharamia asilimia 100 ya gharama za masomo yao.


Kwa mujibu wa Waziri huyo, wanafunzi hao 10 wanaungana na wanafunzi wengine 50 waliotangazwa awali, hivyo kufanya jumla ya wanafunzi watakaonufaika na mpango huo kufikia 60.



Amesema wanufaika hao watasomea fani za Data Science, Artificial Intelligence (Akili Unde) na Allied Sciences, ambazo ni miongoni mwa taaluma zinazolenga kukidhi mahitaji ya ujuzi wa kisasa na kuimarisha uwezo wa Taifa kukabiliana na changamoto za kiteknolojia.


Profesa Mkenda amesema wanafunzi 50 waliopata fursa awali wataanza kambi yao ya mafunzo katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela African Institution of Science and Technology (NM-AIST), Arusha, kuanzia Septemba 14, 2026, huku wakitakiwa kuripoti chuoni hapo Septemba 13, 2026.


Akizungumzia mchakato wa uteuzi, Profesa Mkenda amesema wanafunzi hao walichaguliwa kwa kuzingatia ufaulu wao wa juu katika mitihani ya Kidato cha Sita, hususan katika michepuo ya sayansi ya PCM, PGM na PMC.


Amesema wanafunzi 50 waliokuwa katika nafasi za kwanza hadi ya 50 walichaguliwa kwenda Arusha, huku waliokuwa katika nafasi ya 51 hadi ya 60 wakipata fursa ya kwenda kusoma nchini Urusi.


“Kati ya wanafunzi 10 wanaokwenda Urusi, wanafunzi nane wanatoka katika shule za Serikali na wawili wanatoka shule binafsi,” amesema.


Profesa Mkenda amesisitiza kuwa Serikali imezingatia misingi ya uwazi, usawa na uadilifu katika mchakato wa uteuzi, kwa lengo la kuhakikisha fursa hizo zinawanufaisha wanafunzi wenye uwezo unaostahili.


Aidha, amesema Wizara inaendelea kuratibu maandalizi ya safari ya wanafunzi hao, ikiwamo kuwawezesha kupata pasipoti, ambapo wanafunzi tisa kati yao hawakuwa na pasipoti.


Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wanafunzi hao wanakamilisha maandalizi yote muhimu na kuondoka nchini kwa wakati kuelekea Moscow.


Waziri Mkenda amefafanua kuwa majina ya wanafunzi wote 10 waliochaguliwa yatawekwa kwenye tovuti rasmi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ili kuwawezesha wananchi kupata taarifa zaidi kuhusu wanufaika wa fursa hiyo.





Previous Post Next Post