Na Jasmine Shamwepu Dodoma.📍
Vijana nchini wametakiwa kuongeza ushiriki wao katika mijadala na michakato ya sera ili kuhakikisha changamoto na mahitaji yao yanazingatiwa katika mipango ya maendeleo ya nchi.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Mawasiliano wa Mradi wa **Key Jana Impact**, Erick Malliya, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana yanayofanyika Dodoma, ambapo alisema mradi huo unalenga kuwapatia vijana taarifa na maarifa yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika michakato ya sera na maendeleo.
Malliya ameisema mradi huo ulianzishwa na vijana watano walioshiriki katika mafunzo ya **DANIDA Fellows**, yaliyolenga kuwawezesha vijana kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kuchangia katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Amesema Key Jana Impact inatekelezwa kwa kushirikiana na **ActionAid Tanzania** na kufadhiliwa na Ubalozi wa Denmark nchini Tanzania, ikiwa na lengo la kuziba pengo la taarifa za sera miongoni mwa vijana.
“Mradi huu unalenga kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupata taarifa za sera na kuwapa nguvu kushiriki katika mijadala na michakato mbalimbali ya sera,” alisema.
Amesema mradi huo umefanya shughuli katika maeneo mbalimbali, ikiwemo **Pemba, Kigoma, Ruvuma na Mara**, huku shughuli nyingine zikitarajiwa kufanyika Dar es Salaam na Dodoma.
Malliya amesema vijana wamejengewa uwezo katika maeneo yanayohusu uchumi, mabadiliko ya tabianchi na utawala bora, ili waweze kuelewa sera na kushiriki katika utekelezaji wake kuanzia ngazi za chini.
Alitoa mfano wa Pemba, ambapo vijana walipatiwa elimu kuhusu sera zinazohusu uchumi wa buluu, huku vijana wa Mara wakishirikishwa katika masuala ya uchumi na utawala bora.
“Baadhi ya vijana wameweza kushiriki katika michakato ya sera kuanzia ngazi za vijiji na shehia baada ya kupata taarifa na uelewa kuhusu miongozo mbalimbali ya sera,” alisema.
Kwa upande wake, Mtekelezaji wa Mradi wa Key Jana Impact na DANIDA Fellow, **Thabiti John**, alisema mradi huo umeanzisha majukwaa mbalimbali ya kuwawezesha vijana kupata elimu ya sera na kuifikisha kwa vijana wengine katika maeneo yao.
Amesema katika Mkoa wa Mara, shughuli hizo zimefanyika katika wilaya za **Serengeti, Butiama na Tarime**, ambapo vijana wamepewa elimu kuhusu uchechemuzi wa sera na namna ya kushiriki katika michakato ya maamuzi.
“Tarime ni eneo la mpakani kati ya Tanzania na Kenya, hivyo tumekuwa tukiwapa vijana elimu kuhusu namna wanavyoweza kunufaika na fursa zinazotokana na biashara na shughuli za kiuchumi katika maeneo ya mpakani,” alisema.
John amesema mradi huo pia umefanya shughuli Zanzibar kuhusu uchumi wa buluu na Kigoma, huku lengo likiwa ni kuwafanya vijana kuelewa sera zinazowahusu na kutumia maarifa hayo kuleta mabadiliko katika jamii zao.
Msimamizi na Mfuatiliaji wa Mradi wa Key Jana Impact, **Genila Hiel**, alisema hadi sasa vijana 250 wamefikiwa moja kwa moja kupitia shughuli za kuwajengea uwezo kuhusu sera, ushiriki wa kiraia na michakato ya maamuzi.
Amesema mradi umefanya shughuli katika Mara, Pemba, Ruvuma na Kigoma na unapanga kuendelea na shughuli hizo Dar es Salaam na Dodoma.
“Lengo kubwa ni kuona vijana wanashiriki katika michakato ya kiraia na sera. Mpaka mwisho wa mradi tunatarajia kuwafikia vijana 600,000 moja kwa moja na kwa njia zisizo za moja kwa moja kupitia makongamano, warsha, mikutano na majukwaa mbalimbali ya vijana,” alisema.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo kutoka Pemba, **Abdulbasit Ibrahim Kombo**, alisema mafunzo hayo yamemsaidia yeye na vijana wengine kutambua fursa zilizopo katika uchumi wa buluu na namna ya kuzifikia.
Amesema licha ya Pemba kuzungukwa kwa kiasi kikubwa na bahari, vijana wengi hawakuwa na taarifa za kutosha kuhusu namna ya kutumia rasilimali hiyo kama fursa ya kiuchumi.
“Mradi huu umetuelekeza fursa zilizopo, namna ya kuzifikia na jinsi tunavyoweza kunufaika. Pia nimeweza kusaidia vijana kupata mafunzo kuhusu fursa zilizopo katika uchumi wa buluu,” alisema.
Kombo, ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana katika Shehia ya Mikoroshoni, alisema mafunzo hayo pia yamemuongezea uwezo wa kushughulikia changamoto zinazowakabili vijana katika eneo lake na kuwaunganisha na fursa mbalimbali.
Ushiriki wa Key Jana Impact katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Vijana mjini Dodoma umewezesha vijana na wadau mbalimbali kubadilishana uzoefu kuhusu namna ya kuongeza ushiriki wa vijana katika michakato ya maendeleo.
Maadhimisho hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu “Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana.



