MKURUGENZI MSAIDIZI WA UTAFITI (PCCB) ASISITIZA ELIMU YA ANWANI ZA MAKAZI NA USALAMA WA MTANDAO KWA WAKULIMA.


Na Mwandishi Wetu – WMTH, Nanenane, Nzuguni -Dodoma.📍


 Mkurugenzi Msaidizi wa Utafiti kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) Dkt. John Joseph akiwa na Viongozi wengine wametembelea Banda la Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma, kwa lengo la kujionea hudumaza Kidigitali zinazoratibiwa na Wizara pamoja na mchango wake katika Kuimarisha shughuli za kilimo na uchumi wa Kidigitali kupitia maonesho ya Kimataifa Nanenane.


Akipokea ugeni huo, Afisa TEHAMA kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Stanley Maliwa, alieleza kuwa Mfumo wa Anwani za Makazi unawarahishia wakulima kufika katika maeneo ambayo pembejeo za kilimo zinapatikana, Kufika kwenye Maghala ya kuhifadhi Mazao kurahisisha  au sokoni kwa kutumia Huduma ya Mwelekeo wa NaPA, hatua inayosaidia kuongeza ufanisi na ubora katika shughuli za kilimo na biashara.


Bw. Maliwa aliongeza kuwa Wizara pia inaratibu na kusimamia mifumo ya malipo ya kidijitali ikiwemo Jamii Malipo, unaowapa wakulima uwezo wa kupokea malipo ya bidhaa zao kwa njia salama na rahisi. 


 "Matumizi ya mifumo hiyo yanachangia kukuza uchumi wa kidijitali, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050".


Kwa upande wake, Afisa TEHAMA Bw. Charles Liwongwe alieleza kuwa Wizara inaendelea kutoa elimu ya usalama mtandaoni kwa wananchi, hususan wakulima, ili kuwajengea uwezo wa kujikinga dhidi ya matapeli wa mitandaoni. 


Alifafanua kuwa wananchi wanaweza kuripoti namba zinazotumika kufanya utapeli kupitia namba 15040, hatua inayosaidia kupunguza matukio ya uhalifu wa kimtandao.


Baada ya kupokea maelezo hayo, Dkt. Joseph  alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu Mfumo wa Anwani za Makazi na usalama mtandaoni. 


Alibainisha kuwa bado wananchi wengi hawajafahamu kikamilifu manufaa ya mfumo huo na namna unavyoweza kuboresha shughuli zao za kila siku.


"Elimu hii itawasaidia wakulima kutoa taarifa kwa wataalamu pale yanapotokea magonjwa ya mazao kwa kutumia Mfumo wa Anwani za Makazi, hivyo kuwawezesha wataalamu kufika kwa haraka katika maeneo husika na kutatua changamoto hizo kwa wakati. Hii ni hatua muhimu katika kuongeza tija ya uzalishaji na kuboresha huduma kwa wananchi".


Aidha, alieleza kuwa kuongezeka  elimu ya usalama mtandaoni kutasaidia kupunguza matukio ya utapeli wa fedha kwa wakulima na wananchi kwa ujumla, huku kukichochea matumizi salama ya teknolojia za kidijitali katika kukuza uchumi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.




Previous Post Next Post