LONDO AIPONGEZA TASAC, ASISITIZA THAMANI YA MAZAO KUJENGA UCHUMI WA VIWANDA

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Lazaro Londo (Mb), ameipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kuendelea kusogeza huduma na elimu kwa wananchi na wadau, akisisitiza umuhimu wa taasisi hiyo katika kuwezesha shughuli za biashara na usafirishaji wa bidhaa nchini.


Mhe. Londo ameyasema hayo Agosti 7, 2026, alipokuwa ametembelea banda la Tanzania Shipping Agencies Corporation(TASAC) katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.


Katika ziara hiyo, Naibu Waziri amepata fursa ya kujionea namna TASAC inavyotoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake, ikiwemo kusimamia usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira ya bahari na maziwa nchini, pamoja na huduma zinazohusiana na biashara ya meli.


Akizungumza na waandishi wa habari, Mhe. Londo amesema Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kupitia viwanda, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kujenga uchumi shindani, kuongeza kipato cha wazalishaji na kutengeneza fursa zaidi za ajira kwa Watanzania.


Amesema Serikali, kupitia taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, inaendelea kuhakikisha mazao yanayozalishwa nchini yanachakatwa na kuongezewa thamani kabla ya kuingia sokoni, ili yaweze kuwa na ubora na ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi.


Kwa mujibu wa Londo, taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara hiyo, zikiwemo BRELA, TBS, Tume ya Ushindani (FCC), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), SIDO na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), zinaendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia utoaji wa elimu, usajili wa biashara, viwango vya ubora na huduma nyingine zinazolenga kuwawezesha wazalishaji na wafanyabiashara kushiriki kikamilifu katika uchumi wa viwanda.


Aidha, amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa kuimarisha miundombinu ya barabara, madaraja, vivuko, umeme kupitia REA pamoja na miundombinu ya mawasiliano.


Amesema uwekezaji huo unalenga kupunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa, huku ukirahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za masoko kwa wananchi na kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji na biashara.


Mhe. Londo amewataka wananchi kutumia fursa ya Maonesho ya Nanenane kutembelea banda la Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na taasisi zake ili kupata elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa.


Amesisitiza kuwa kuongeza thamani ya mazao ni hatua muhimu katika kuimarisha viwanda vya ndani, kuongeza kipato cha wananchi, kuongeza ajira na kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uzalishaji wa bidhaa zenye ushindani.




Previous Post Next Post