WANANCHI WAPONGEZA BRELA KWA HUDUMA ZA HARAKA, WAHAMASISHA USAJILI WA BIASHARA

 


Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍


Wananchi waliotembelea banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) wamepongeza ubora wa huduma zinazotolewa na wakala huo, wakisema zimekuwa za haraka, rahisi na zenye kutoa elimu inayowasaidia kuelewa taratibu za usajili wa biashara na upatikanaji wa leseni.


Wakizungumza Julai 8, 2026, wananchi hao walisema wamepata mwongozo muhimu unaowawezesha kuanzisha na kusajili biashara zao kwa urahisi, hatua ambayo itawasaidia kujiajiri, kupanua shughuli zao za kiuchumi na kufanya biashara kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.


Mfanyabiashara Abdulheri Misana alisema elimu na ushauri alioupata katika banda la BRELA umemwezesha kuelewa mchakato wa usajili wa biashara pamoja na namna ya kupata leseni kwa wakati, jambo litakalosaidia kukuza biashara yake.


Alieleza kuwa hapo awali alikuwa akikumbana na changamoto katika kupata huduma, lakini baada ya kutembelea banda hilo alipata msaada wa karibu na maelekezo yaliyomwezesha kukamilisha usajili wake kwa urahisi na kwa muda mfupi.


Naye mkazi wa Dar es Salaam, Favid Mwandiki, alisema maboresho yaliyofanywa na BRELA katika mifumo ya utoaji huduma yameongeza ufanisi na kupunguza muda wa kusubiri huduma.



Alisema licha ya kuwepo changamoto chache, hatua zilizochukuliwa zimeleta mabadiliko makubwa, akibainisha kuwa aliweza kukamilisha huduma zote alizohitaji ndani ya takribani dakika 30, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.


Kwa upande wake, Suleiman Fupi, ambaye pia ni mkazi wa Dar es Salaam, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kusajili biashara zao na kujiunga na mfumo rasmi wa biashara ili kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali, ikiwemo kupata huduma kwa urahisi, kushiriki katika zabuni na kupata mazingira bora ya kukuza biashara zao.


Alisema ameridhishwa na kiwango cha huduma alichopata, akisisitiza kuwa maboresho ya mifumo ya BRELA yameongeza kasi, uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma za usajili wa biashara na leseni, jambo linaloimarisha mazingira ya kufanya biashara nchini.

Previous Post Next Post