Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Tamasha la 17 la Muziki wa Cigogo litakalofanyika Julai 25, 2026 katika viwanja vya Chamwino Arts Centre (CAC), Chamwino Ikulu, jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa Chamwino Arts Centre, Naamala Samson, alisema maandalizi ya tamasha hilo yamekamilika na kwamba kila kitu kiko tayari kwa ajili ya kuwapokea wageni kutoka ndani na nje ya Tanzania katika maadhimisho hayo ya siku tatu yanayofanyika kuanzia Julai 24 hadi 26.
Naamala alisema tamasha hilo limefikia mwaka wake wa 17, jambo ambalo linaonyesha mafanikio makubwa katika juhudi za kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa Kigogo pamoja na urithi wa Tanzania kwa ujumla.
"Tunafurahi sana kufikia hatua hii ya kuadhimisha Tamasha la 17 la Muziki wa Utamaduni wa Cigogo. Tunawaalika Watanzania wote kufika Chamwino Arts Centre kushuhudia urithi wetu wa kipekee na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu tamaduni zetu," alisema.
Alieleza kuwa wageni watakaofika katika tamasha hilo watapata fursa ya kushuhudia maonesho ya ngoma za asili kutoka maeneo mbalimbali, zitakazotumika kuhamasisha jamii kuendelea kuhifadhi mila, desturi na utamaduni wa Tanzania.
Mbali na burudani za muziki na ngoma za asili, tamasha hilo pia litakuwa na maonesho ya vyakula vya asili pamoja na mashindano ya upishi yatakayowakutanisha wapishi kutoka maeneo mbalimbali, huku wananchi wakipata nafasi ya kuonja vyakula hivyo.
Naamala alisema tamasha hilo limewashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo na taasisi zinazotoa huduma kwa wananchi. Miongoni mwao ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ambalo litatoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuandaa mashindano yatakayowawezesha washindi kujishindia majiko ya kisasa yanayotumia nishati safi.
Aliongeza kuwa wananchi watakaotembelea banda la TANESCO watapata elimu kuhusu matumizi ya nishati safi pamoja na fursa ya kuonja vyakula vilivyopikwa kwa kutumia teknolojia hiyo.
Wadau wengine watakaoshiriki katika tamasha hilo ni pamoja na CRDB Bank Plc, Alliance Française, BASATA, COSOTA, Kayingi Arts, Chamwino Connect, Uswazi Born Talent, East Africa Protocol Services (EAPS), Innovative Development for Future Generation (IDFG), Bodi ya Filamu Tanzania, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, MDACHI Tech, Polisi Tanzania kupitia Dawati la Jinsia, Master Tents, SHISAMA, Arterial Network Tanzania na TAKUKURU, ambao watatoa huduma na elimu mbalimbali kwa wananchi.
Naamala aliwataka Watanzania kutoka kila kona ya nchi kutumia fursa hiyo kutembelea tamasha hilo, akibainisha kuwa Dodoma sasa inafikika kwa urahisi kupitia reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam na mikoa mingine.
"Tunawakaribisha Watanzania wote na wageni kutoka nje ya nchi kuja kushuhudia uzuri wa utamaduni wa Cigogo pamoja na shughuli mbalimbali zitakazofanyika katika siku hizi za tamasha hapa Chamwino Arts Centre," alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, ambaye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa tamasha hilo, ameipongeza Chamwino Arts Centre kwa kuendelea kuandaa tamasha hilo ambalo limekuwa jukwaa muhimu la kutangaza utamaduni wa Kigogo na vivutio vya Tanzania kimataifa.
Amesema ushiriki wa wageni kutoka mataifa mbalimbali unaonyesha jinsi tamasha hilo linavyoendelea kukuza utalii wa utamaduni na kuitangaza Tanzania duniani kupitia sanaa, muziki na urithi wa jadi.
Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zinazolenga kuhifadhi tamaduni za Watanzania huku zikichochea maendeleo ya uchumi kupitia sekta ya utamaduni na utalii.




