NACTVET: ELIMU YA AMALI YAANZA KUZAA WAAJIRI, SI WATAFUTA AJIRA

 


Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍


Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya 

Ufundi Stadi (NACTVET) limesema utekelezaji wa sera iliyoboreshwa ya elimu umeanza kuleta matokeo chanya, huku wanafunzi wa elimu ya amali na ufundi wakionyesha uwezo mkubwa wa kubuni bidhaa na huduma zinazowawezesha kujiajiri na hata kuajiri wengine.


Akizungumza leo Julai 12, 2026, baada ya kutembelea Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la NACTVET, Bi. Bernadetta Ndunguru, alisema maonesho ya mwaka huu yameonyesha wazi kuwa elimu ya amali imeanza kubadili mtazamo wa vijana kutoka kutegemea ajira hadi kuwa wabunifu na watengeneza fursa za ajira.


Alisema ushahidi wa mafanikio hayo umeonekana kupitia kazi za wanafunzi wa Kidato cha Tatu wanaosoma elimu ya amali, ambao wamewasilisha bunifu zenye thamani ya kiuchumi na uwezo wa kutatua changamoto za jamii.


Ndunguru alimtaja mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Amali Bwiru mkoani Mwanza aliyebuni mfano wa nyumba ya gharama nafuu unaoonyesha hatua zote za ujenzi pamoja na makadirio ya gharama, huku ubunifu huo ukiwa tayari umeanza kumuingizia kipato.


Aidha, alisema mwanafunzi mwingine wa mkondo wa TEHAMA ameunda programu inayowasaidia wafanyabiashara wadogo kurekodi mapato, matumizi na faida kwa urahisi, ambapo programu hiyo tayari imeanza kuuzwa sokoni.



Mbali na bunifu za wanafunzi, Ndunguru alisema taasisi zilizo chini ya usimamizi wa NACTVET, zikiwemo DIT, NIT na VETA, zinaendelea kutoa mafunzo yanayolenga kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kuanzisha biashara, kampuni na viwanda vyao wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa.


Aliongeza kuwa katika ziara yake katika banda la DIT alishuhudia ubunifu wa kutengeneza vipuri vya bajaji kwa kutumia chupa za plastiki zilizotumika, jambo linaloonyesha uwezo wa Watanzania kubuni teknolojia na bidhaa zinazoweza kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.


Ndunguru alisema mafanikio hayo yanaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza ujenzi wa uchumi wa viwanda unaotegemea ubunifu, ujuzi na ujasiriamali.


Alisisitiza kuwa NACTVET itaendelea kusimamia utoaji wa mafunzo yanayozalisha wahitimu wenye uwezo wa kuwa waajiri, wabunifu na waanzilishi wa viwanda, hatua ambayo itachochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira nchini.



Previous Post Next Post