Na Carlos Claudio, Dar es Salaam.📍
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema mfumo wa kidijitali wa Sema na BoTumeleta mageuzi katika upokeaji wa malalamiko kutoka kwa wateja na watoa huduma za kifedha, kwa kurahisisha mawasiliano na kuongeza kasi ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili.
Tutuba alitoa kauli hiyo alipotembelea banda la BoT katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo alisema mfumo huo umewezesha wananchi kuwasilisha malalamiko yao moja kwa moja bila kupitia taratibu ndefu, hatua ambayo imeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Alisema kupitia mfumo huo, wateja na watoa huduma za kifedha wanaweza kujisajili kwa urahisi na kuwasilisha malalamiko yao kidijitali, jambo linalorahisisha ufuatiliaji na kuhakikisha changamoto zinashughulikiwa kwa wakati.
"Kupitia mfumo huu, sasa wateja na watoa huduma za kifedha wanaweza kujisajili moja kwa moja na kuwasilisha malalamiko yao kwa urahisi," alisema Tutuba.
Aidha, alisisitiza kuwa BoT inaendelea kuimarisha mifumo ya kisasa ya usalama wa taarifa ili kuhakikisha taarifa za watumiaji wa huduma za kifedha zinabaki salama na kulindwa dhidi ya matumizi yasiyoidhinishwa.
Alieleza kuwa maboresho hayo yanalenga kuhakikisha kila mteja anafanya miamala yake kwa usalama, bila hofu ya taarifa zake muhimu kufikiwa na watu wasiohusika.
Tutuba aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia katika sekta ya fedha ni sehemu ya juhudi za BoT za kuboresha huduma, kuongeza uwazi na kujenga imani kwa wananchi wanaotumia huduma za kifedha nchini.
