Na Carlos Claudio, Chamwino.📍
Kampuni ya Bonite Bottles Limited imesema ushiriki wake katika Tamasha la 17 la Muziki wa Cigogo unalenga kuwatambulisha wananchi chapa yake mpya ya Kilimanjaro Natural Mineral Water, sambamba na kuwapa fursa ya kufurahia ladha halisi ya maji hayo wakati wa tamasha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 24, 2026 katika viwanja vya Chamwino Arts Centre, Afisa Masoko wa Bonite Bottles Limited Mkoa wa Dodoma, Samwel Masawe, alisema kampuni hiyo imeamua kuwa sehemu ya tamasha hilo ikiwa ni sehemu ya kuendelea kusogeza bidhaa zake karibu na wateja na kuunga mkono maendeleo ya sanaa na utamaduni nchini.
Masawe alisema wananchi watakaohudhuria Tamasha la 17 la Muziki wa Cigogo watapata nafasi ya kuonja na kujionea ubora wa Kilimanjaro Natural Mineral Water, huku pia wakielimishwa kuhusu mabadiliko ya jina la bidhaa hiyo kutoka Kilimanjaro Drinking Water kwenda Kilimanjaro Natural Mineral Water.
"Tunashiriki tamasha hili ili kuwapatia wananchi ladha halisi ya maji yetu ya Kilimanjaro Natural Mineral Water na pia kuwafahamisha kuhusu utambulisho wetu mpya wa bidhaa. Mabadiliko haya yanaakisi ubora na asili ya maji tunayozalisha," alisema Masawe.
Aliongeza kuwa Bonite Bottles Limited imekuwa na utamaduni wa kudhamini matamasha na matukio mbalimbali nchini kama sehemu ya mchango wake katika kukuza vipaji, sanaa, utamaduni na kuimarisha ushirikiano na jamii.
Tamasha la 17 la Muziki wa Cigogo linatarajiwa kufunguliwa rasmi kesho, Julai 25, 2026, katika viwanja vya Chamwino Arts Centre, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi. Tamasha hilo linatarajiwa kukutanisha wasanii wa muziki wa asili, wadau wa utamaduni na maelfu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.



