Na amwandishi Wetu
Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Zainab Khamis Shomari, ameihimiza Serikali kupitia Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) kuendelea kuimarisha utekelezaji wa mpango wa mikopo nafuu wa Mwinyi Boost Fund ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususani wajasiriamali na makundi ya kipato cha chini.
Mhe. Zainab amesema kuwa Serikali ilitenga Shilingi Bilioni 3.5 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo, lakini hadi sasa kiasi cha Shilingi Bilioni 2 pekee ndicho kilichotumika, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo hiyo ili fedha zilizotengwa ziweze kuwanufaisha wananchi waliokusudiwa.
Ameeleza kuwa Mwinyi Boost Fund imeendelea kuwa mkombozi kwa wajasiriamali wadogo, vijana, wanawake na wananchi wa kipato cha chini kwa kuwapa fursa ya kupata mitaji nafuu na hivyo kukuza shughuli zao za kiuchumi na kuongeza kipato cha familia zao.
Aidha, Mhe. Zainab amesema kuwa kuanzishwa kwa mfuko huo kunatokana na dhamira ya dhati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ya kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi Zanzibar.
Mhe. Zainab aliyasema hayo Juni 7, 2026, katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani, Zanzibar, alipokuwa akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
