WANANCHI DODOMA WAIPONGEZA BODI YA KOROSHO KWA KUTOA MAFUNZO YA KILIMO BORA CHA KOROSHO


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Wananchi na wakulima wa zao la korosho mkoani Dodoma wameipongeza Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Liyendele pamoja na TPHPA kwa kutoa mafunzo ya kilimo bora cha korosho yaliyosaidia kuongeza uelewa wa wakulima kuhusu uzalishaji wa zao hilo.


Mafunzo hayo yaliyofanyika katika halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Dodoma yalilenga kuwajengea uwezo wakulima kuhusu matumizi sahihi ya viwatilifu, udhibiti wa magonjwa na wadudu pamoja na mbinu bora za uzalishaji wa korosho.


Wakizungumza baada ya mafunzo hayo, baadhi ya wakulima wa Wilaya ya Mpwapwa walisema elimu waliyoipata itawasaidia kuongeza uzalishaji pamoja na kuboresha mashamba yao ya korosho.



Mkulima wa zao la korosho, Bosco Mesela, alisema mafunzo hayo yamewapa uelewa mkubwa wa namna ya kutumia viwatilifu kwa usahihi na wakati sahihi ili kuzuia magonjwa na wadudu wanaoharibu mikorosho.


“Tunaishukuru sana Bodi ya Korosho, TARI pamoja na TPHPA kwa kutuletea mafunzo haya muhimu. Tumepata elimu kubwa ambayo itatusaidia kuongeza tija kwenye kilimo chetu cha korosho,” alisema Mesela.



Naye mkulima mwingine, Modesta Muhamilawa, alisema mafunzo hayo yamewasaidia wakulima wengi ambao awali hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu kilimo cha korosho.


Alisema kupitia elimu hiyo sasa wakulima wataweza kusimamia vizuri mashamba yao na kuongeza uzalishaji wa zao hilo ambalo linaendelea kuwa tegemeo kwa wananchi wengi wa Mkoa wa Dodoma.



Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mpwapwa Mjini, George Fuime, alisema ujio wa wataalamu hao umeleta mwamko mkubwa kwa wakulima wa eneo hilo na kusaidia kuongeza hamasa ya kulima korosho kwa tija.


“Awali wakulima wengi walikuwa hawana elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya pembejeo na namna bora ya kutunza mikorosho, lakini sasa wamepata uelewa mkubwa kupitia mafunzo haya,” alisema Fuime.



Mwakilishi kutoka Bodi ya Korosho Tanzania Makao Makuu Mtwara, Pafra Masele, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wakulima wanapata elimu sahihi ya kilimo bora cha korosho pamoja na matumizi salama ya viwatilifu.


Alisema Bodi ya Korosho itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wakulima wanapata elimu itakayowawezesha kuongeza uzalishaji na kipato.



Naye Mtafiti kutoka TARI Liyendele, Abdallah Makale, alisema wakulima wengi wa Dodoma walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya kutofahamu namna bora ya kudhibiti magonjwa na wadudu wa korosho, hivyo mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa kwao.


Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Mpwapwa, Mguto Mathew, aliwashukuru wataalamu hao kwa kufika Dodoma na kutoa elimu ambayo alisema itasaidia kuongeza tija kwa wakulima pamoja na kukuza uchumi wa wananchi wa kanda ya kati.



Alisema Mkoa wa Dodoma una uwezo mkubwa wa kuzalisha korosho na kupitia elimu hiyo wakulima wataweza kulitumia vizuri zao hilo kama chanzo cha mapato na maendeleo.














🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post