Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Wiki ya Saratani ya Macho kwa Watoto, huku wazazi na walezi wakitakiwa kuongeza umakini katika kufuatilia afya ya macho ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano ili kubaini mapema dalili za saratani ya jicho aina ya Retinoblastoma.
Wito huo umetolewa leo Mei 15, 2026 jijini Dodoma na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Elihudi Eliakimu, aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, wakati wa maadhimisho ya wiki hiyo yaliyofanyika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Dkt. Eliakimu amesema saratani hiyo inaweza kutibika iwapo mtoto atagundulika mapema na kuwahi kufikishwa katika vituo vya huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu, akisisitiza kuwa kuchelewa kugundua dalili za ugonjwa huo kunachangia kuongezeka kwa vifo na upofu kwa watoto.
Amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu saratani ya macho kwa watoto, sambamba na kuhamasisha familia na walezi kuwapeleka watoto hospitalini mara wanapoona mabadiliko yoyote kwenye macho yao.
“Saratani hii hutokea zaidi kwa watoto chini ya miaka mitano na inaweza kuathiri jicho moja au yote mawili. Ikiachwa bila matibabu huweza kuharibu jicho lote, kulazimisha kuondolewa kwa jicho au hata kusababisha kifo,” amesema Dkt. Eliakimu.
Aidha, amesema tafiti zinaonesha kuwa watoto wengi nchini hufikishwa hospitalini kuchelewa, ambapo baadhi yao huwasili katika vituo vya afya takribani miezi 10 baada ya kuanza kuonesha dalili za awali za ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, mtoto mmoja kati ya watoto hai 18,000 huzaliwa akiwa na saratani hiyo ya macho, huku tafiti za Afrika zikionesha kuwa ni asilimia 20 hadi 48 pekee ya watoto wanaogundulika na ugonjwa huo wanaofanikiwa kuishi kwa zaidi ya miaka mitano baada ya kugundulika.
Dkt. Eliakimu amewataka wazazi kuhakikisha watoto wao wanapimwa macho angalau mara moja kwa mwaka ili kubaini mapema changamoto zinazoweza kujitokeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Hamad Nyembea, amesema katika mwaka 2025 watoto zaidi ya laki mbili walifanyiwa uchunguzi wa macho nchini, ambapo asilimia 39 walibainika kuwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanayoathiri macho.
Amesema serikali imeendelea kuimarisha huduma za macho nchini kupitia hospitali za mikoa, ambapo kati ya hospitali 28 za mikoa za serikali, hospitali 21 tayari zina wataalamu bingwa wa macho.
“Hivi sasa tuna jumla ya mabingwa 31 wa macho katika hospitali za mikoa, hatua ambayo imeongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa kwa wananchi,” amesema Dkt. Nyembea.
Aidha, amesema huduma za magonjwa ya macho zinahitaji uwekezaji mkubwa, huku Shirika la Afya Duniani (WHO) likipendekeza kuwepo kwa hospitali maalum ya huduma za kibobezi za macho kwa watoto kwa kila watu 10,000.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Henry Humba, amesema hospitali hiyo imebaini wagonjwa saba wa saratani ya Retinoblastoma, ambapo watoto watatu wamepatiwa matibabu na kupona.
Amesema kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma za macho, hospitali hiyo inapanga kujenga jengo maalum kwa ajili ya huduma na mafunzo ya magonjwa ya macho, ikiwemo Retinoblastoma.
“Takwimu zinaonesha kuwa watoto kati ya 100 hadi 150 huonekana kila mwaka nchini wakiwa na tatizo la Retinoblastoma, hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuongeza huduma na vifaa tiba,” amesema Dkt. Humba.
Kwa upande wake, mzazi wa mtoto anayekabiliwa na saratani ya macho, Judith Mollel, ameomba serikali kuingiza huduma za uchunguzi wa macho katika kliniki za mama na mtoto (RCH) pamoja na kwenye kadi za kliniki ili kusaidia kubaini mapema changamoto hiyo kwa watoto.
Amesema wazazi wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu dalili za awali za ugonjwa huo, hali inayochangia kuchelewa kwa watoto kufikishwa hospitalini.
Wiki ya Saratani ya Macho kwa Watoto mwaka huu imebeba kaulimbiu isemayo; “Saratani ya Macho kwa Watoto, Umoja katika Upekee.”
🚨Full VIDEO Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA










