Na. Mwandishi Wetu, DODOMA📍
Mwenge wa Uhuru 2026, wazindua Mradi wa Nishati Safi na Klabu ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Shule ya Sekondari Dr. Samia-Dodoma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2026, Wazo Mwang’onda aliipongeza serikali kwa kutekeleza mradi wa Nishati safi unaochangia utunzaji wa mazingira kupitia uzalishaji wa biogesi inayotumika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kupikia.
Alisema kuwa ni Nishati safi itiliwe mkazo zaidi ili kuinusuru jamii na mabadiliko hasi ya kimazingira. "Mradi huu unasaidia kulinda mazingira na kupunguza gharama za matumizi ya nishati, ambapo shule inaokoa takribani shilingi milioni 12 kwa mwaka ambazo zingetumika kununua nishati nyingine” alisema Mwang’onda.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Dr. Samia, Mwl. Leticia Singo alisema kuwa serikali kupitia Wizara ya Elimu chini ya Mradi wa P4R ilitoa shilingi 698,800,161.86 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. Alisema kuwa mradi huo umeongeza ufanisi katika utendaji wa shughuli za shule huku ukichangia mazingira safi na salama kwa wanafunzi na watumishi.
Nae, mwanafunzi wa shule hiyo alisema uzinduzi wa klabu ya kupambana na rushwa umewapa elimu na hamasa ya kupinga rushwa, akibainisha kuwa “rushwa ni adui wa haki”
Uzinduzi wa mradi huo na klabu ya kupambana na rushwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kuhamasisha matumizi ya Nishati safi pamoja na kujenga kizazi cha vijana wenye maadili na uzalendo.






