MAKONDA AZINDUA OFISI ZA JUMIKITA DODOMA, AHIMIZA MATUMIZI SAHIHI YA MITANDAO YA KIJAMII

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amezindua ofisi mpya za Jumuiya ya Wanahabari ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA), Tawi la Dodoma, na kuitaka jumuiya hiyo kutumia mitandao ya kijamii kujenga jamii yenye maadili pamoja na kulinda utamaduni wa Kitanzania kupitia matumizi sahihi ya Kiswahili.


Akizungumza Mei 3, 2026 katika eneo la Ilazo jijini Dodoma, Makonda amesema kuwa mitandao ya kijamii ina mchango mkubwa katika kuelimisha jamii na kukuza maendeleo, hivyo inapaswa kutumika kwa uwajibikaji badala ya kusambaza maudhui yanayoharibu maadili ya taifa.


Amesisitiza kuwa Kiswahili ni sehemu muhimu ya utambulisho wa taifa la Tanzania na Afrika kwa ujumla, akibainisha kuwa kupitia ushirikiano na UNESCO, Tanzania imeendelea kupata heshima kubwa duniani katika kukuza na kuendeleza lugha hiyo.


Makonda ameongeza kuwa Tanzania inatarajia kushiriki katika maadhimisho ya Kiswahili duniani yatakayofanyika Paris, hatua inayodhihirisha nafasi ya nchi katika kukuza lugha hiyo kimataifa.



Katika hotuba yake, Waziri huyo amewataka wanamitandao kuwa mabalozi wa maadili kwa kuhakikisha maudhui wanayochapisha yanazingatia mila, desturi na misingi ya jamii ya Kitanzania.


“Tunataka mitandao itumike kujenga taifa letu, kuonesha fursa zilizopo nchini na kuhamasisha maendeleo ya jamii,” amesema Makonda.


Aidha, amesisitiza umuhimu wa wanahabari na watengeneza maudhui kufanya kazi kwa weledi na kuepuka kusambaza taarifa zinazochochea migogoro kwa maslahi binafsi.


Kwa upande mwingine, amesema Serikali itaendelea kuwawezesha vijana wa mitandao kwa kuwapatia mikopo na fursa mbalimbali ili kukuza kazi zao na kuchangia maendeleo ya taifa.


Makonda amepongeza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango kwa vijana wa mitandao, ili waweze kutumia vipaji vyao kukuza uchumi na kuitangaza Tanzania kimataifa.


Pia ametoa wito kwa JUMIKITA kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda maadili, kuhamasisha uzalendo na kuhakikisha mitandao ya kijamii inatumika kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.



🚨Full Video Inapatikana katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post