Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imetangaza kuandaa kongamano lake la kwanza la kisayansi kuhusu upandikizaji wa viungo, likilenga kuleta mwelekeo mpya wa huduma hiyo nchini sambamba na maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 5, 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi, amesema kongamano hilo litafanyika kesho katika ukumbi wa Domia Estate, likihusisha wataalamu wa afya pamoja na wananchi.
Amesema maadhimisho ya miaka 10 ya hospitali hiyo yalianza Oktoba 13, 2015 na yatahitimishwa rasmi Julai 15 mwaka huu, huku kongamano hilo likiwa sehemu ya kilele cha matukio muhimu.
“Kongamano hili lina lengo la kutoa mwelekeo wa huduma za upandikizaji viungo nchini, kufanya tathmini ya tulipo na tunakoelekea, pamoja na kutoa ushauri kwa Wizara ya Afya Tanzania,” amesema Prof. Makubi.
Ameongeza kuwa kongamano hilo pia litatoa fursa ya kubadilishana uzoefu kati ya wataalamu wa ndani na nje ya nchi, ambapo washiriki kutoka Uganda, Nigeria, Italia, Japan, Afrika Kusini na Uingereza watashiriki kwa njia ya mtandao.
Kwa mujibu wa Prof. Makubi, hospitali hiyo tayari imepiga hatua katika huduma za upandikizaji wa figo na uroto (bone marrow), huku pia ikisaidia kujenga uwezo kwa hospitali nyingine kama Bugando.
Amesema moja ya malengo ya kongamano hilo ni kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uchangiaji wa viungo (organ donation), pamoja na kutangaza upatikanaji wa huduma hizo nchini.
“Kongamano hili pia litafungua milango ya ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya afya, sambamba na jitihada za Serikali za kupanua huduma za kibingwa,” ameongeza.
Zaidi ya washiriki 150 wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo, huku wananchi wakihimizwa kufuatilia na kushiriki ili kuongeza uelewa wao.
Katika hatua nyingine, BMH imeanzisha kampeni ya kuhamasisha wadau kuchangia mfuko wa upandikizaji viungo, ili kuwasaidia wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Prof. Makubi amesema hadi sasa hospitali hiyo imefanikiwa kufanya upandikizaji wa figo zaidi ya 40 na uroto zaidi ya 70, huku mahitaji ya huduma hiyo yakiendelea kuongezeka.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji na Rais wa Chama cha Madaktari katika hospitali hiyo, Dkt. Mugisha Mkoronko, amesema uwekezaji uliofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Afya umewezesha utoaji wa huduma hizo nchini, badala ya wagonjwa kusafiri nje ya nchi.
“Kwa sasa zaidi ya wagonjwa 56 waliopandikizwa figo wanaendelea vizuri, na tunatarajia makongamano yajayo kuwa ya kimataifa zaidi,” amesema Dkt. Mkoronko.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu na Upandikizaji Uroto, Dkt. Stella Malangahe, amesema mahitaji ya huduma hiyo ni makubwa hasa kwa watoto, ambapo tayari watoto 30 wamefanyiwa upandikizaji huo.
Amesema hospitali hiyo inapanga kupanua wodi ya wagonjwa kutoka vyumba vitatu hadi sita, pamoja na kuboresha miundombinu ya huduma ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
“Tumelenga kuanza na magonjwa yasiyo ya saratani, lakini tunapanua wigo ili kujumuisha pia magonjwa ya saratani yanayoathiri watoto,” amesema Dkt. Malangahe.
BMH imeeleza kuwa kupitia juhudi hizo, inalenga kuimarisha huduma za kibingwa nchini na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata matibabu ya kisasa bila kulazimika kusafiri nje ya Tanzania.
🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu ya WASHINDI MEDIA
