TBS YATANGAZA “VIWANGO MARATHON” YA KIHISTORIA



Na Mwandishi Wetu, Dodoma.📍


Mwamko wa wananchi kushiriki mashindano ya marathon nchini umeendelea kuongezeka kwa kasi, huku watu wa rika mbalimbali pamoja na wanariadha kutoka mataifa jirani wakionesha hamasa kubwa ya kushiriki mbio hizo.


Hali hiyo imejidhihirisha katika Bunge Marathon iliyofanyika Aprili 18,2026 katika viwanja vya Jamhuri Jijini Dodoma. 


Mwanariadha na Mhariri kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Isakwisa Mbyale amesema uzoefu walioupata katika Bunge Marathon umeongeza hamasa kwa TBS kuandaa “Viwango Marathon” itakayofanyika Mei 31 katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.


Amesema tofauti kubwa ya marathon hiyo ni msisitizo wa ubora na usahihi wa viwango katika kila hatua ya mashindano, hususani kwenye ruti za mbio.



“Katika marathon kuna umbali tofauti kama kilometa 5, 10, 21 na zaidi. Ni muhimu kuhakikisha mshiriki anakimbia umbali halisi uliopangwa. Haiwezekani mtu aandikwe kilometa 21 halafu akimbie 25. Hapo viwango vinakuwa havijazingatiwa,” ameema.


Ameeleza kuwa TBS kama taasisi inayosimamia ubora wa bidhaa na huduma mbalimbali nchini, imeamua kuhamishia dhana hiyo pia kwenye michezo kwa kuhakikisha Viwango Marathon inakuwa mfano wa mashindano yenye ubora wa hali ya juu.



“Tunataka kila kitu kiwe cha kiwango. Kuanzia maandalizi, usimamizi wa mbio, hadi vifaa vinavyotolewa. Ndiyo maana tumeita Viwango Marathon,” amesisitiza.


Pia ametoa wito kwa Watanzania pamoja na wadau wa michezo kutoka ndani na nje ya nchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano hayo ambayo yanatarajiwa kuwa miongoni mwa marathon zenye ushindani mkubwa na viwango bora zaidi nchini.


“Tunakaribisha kila mtu, vijana, wazee, watoto na wanariadha wa kitaalamu. Hii ni marathon ya watu wote, lakini yenye viwango vya juu,” amesema.


Viwango Marathon inatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuhamasisha afya, michezo na mshikamano wa kijamii, huku ikiweka mfano mpya wa mashindano ya riadha yanayozingatia ubora na usahihi nchini Tanzania.

Previous Post Next Post