JAMII MTWARA YASISITIZWA MATUMIZI SAHIHI YA DAWA.

 


Jamii ya Mkoa wa Mtwara imesisitizwa kuzingatia matumizi sahihi ya dawa kama njia muhimu ya kulinda afya binafsi na ya umma, kupitia ziara ya uelimishaji na uhamasishaji iliyoendeshwa Aprili 20, 2026 na Baraza la Famasi kwa kushirikiana na Idara ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya.


Hayo yamesemwa na Msajili wa Baraza la Famasi, Bw. Boniface Magige, alipokuwa akizungumza na wataalam wa kada ya famasi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara - Ligula, ambapo aliwakumbusha wajibu wao wa kuhakikisha wanatoa elimu sahihi kwa jamii na kusimamia matumizi salama ya dawa ili kuepusha madhara yanayoweza kuzuilika.


Katika ziara hiyo, wataalam wa kada ya famasi wakiwemo wafamasia watarajali (interns) walipata maelekezo mbalimbali ya kitaalamu kuhusu namna bora ya kuhudumia wagonjwa na kusisitiza matumizi sahihi ya dawa.


Aidha, Mwenyekiti wa Baraza la Famasi, Mfamasia Jafary Liana, alieleza umuhimu wa mafunzo kwa vitendo (internship training) katika kuwajengea wataalam umahiri na ufanisi katika utoaji wa huduma za kifamasia.

Sambamba na hilo, elimu kuhusu matumizi sahihi ya dawa ilitolewa kwa wagonjwa waliofika kupata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara - Ligula, wakikumbushwa kufuata maelekezo ya wataalam wa afya, kuepuka matumizi holela ya dawa, na kukamilisha dozi kama ilivyoelekezwa.


Kadhalika, timu ya uelimishaji iliwafikia wanafunzi wa Shule ya Sekondari Sabasaba, ambapo walipewa elimu juu ya madhara ya matumizi holela ya dawa pamoja na utaratibu sahihi wa kujiunga na masomo ya fani ya famasi katika elimu ya juu.

Ziara hiyo imelenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu matumizi sahihi ya dawa, kupunguza madhara yatokanayo na matumizi holela, na kuimarisha afya ya wananchi kwa ujumla.


#MatumiziSahihiYaDawa  #WizaraYaAfya #BarazaLaFamasi #ElimuKwaUmma





🚨Subscribe YOUTYBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post