Na Jasmine Shamwepu, Dodoma.📍
Mkurugenzi wa Shirika la Vijana wa Tanzania kwa Ujenzi wa Taifa (TAYNACO), Masasila Kadoke, amezindua rasmi shirika hilo kwa lengo la kuongeza matumaini kwa vijana, kuimarisha mshikamano wao na kujenga uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Kadoke amesema kuanzishwa kwa TAYNACO kunatokana na uhitaji wa dhati wa kuwa na jukwaa la pamoja litakalowaunganisha vijana, kusikiliza changamoto zao na kutoa suluhisho la vitendo bila kuegemea upande wowote wa kisiasa.
Amesema kupitia shirika hilo, vijana wanatarajiwa kunufaika kiuchumi kwa kutumia fursa mbalimbali zitakazotolewa, huku akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuongeza kasi ya matumaini na maendeleo kwa vijana nchini.
Katika kufanikisha malengo yake, Kadoke ameeleza kuwa TAYNACO imejipanga kutekeleza programu na mifumo mbalimbali, ikiwemo mfumo wa kuwaunganisha vijana na fursa zilizopo nchini, ambao utakuwa daraja muhimu kati ya vijana na nafasi za kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TAYNACO, Sadick Augustino, amesema shirika hilo litahakikisha linakuwa sauti ya vijana kwa kuwasikiliza na kuwashirikisha kikamilifu katika mchakato wa maendeleo ya Taifa.
Aidha, amewataka vijana kuwa tayari kuchangamkia fursa zitakazopatikana, huku akibainisha kuwa wataalam wa sheria ndani ya shirika hilo watahakikisha kunakuwepo ulinzi wa kisheria kwa vijana ili kulinda maslahi mapana ya Taifa.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA

