KUZINGATIA RATIBA ZA CHANJO NI KINGA MADHUBUTI KWA MTOTO.


📌Na Elimu ya Afya kwa Umma.


Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo imeendelea kusisitiza umuhimu wa kufuata ratiba za chanjo kwa watoto, hatua inayolenga kuwalinda dhidi ya magonjwa hatari yanayozuilika kwa chanjo.


Akizungumza leo tarehe 30,Machi,2026  Jijini Arusha wakati wa Mafunzo kwa Viongozi Wasimamizi Huduma za Chanjo (Mid-level Managers - Training on Immunization Services 

 MLM)  yaliyowahusisha washiriki kutoka mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga, Afisa Afya kutoka Mpango wa Taifa wa Chanjo, Wizara ya Afya, Bw. Bonventure Nestory amesema kuwa uzingatiaji wa ratiba za chanjo ni nguzo muhimu katika kuhakikisha watoto wanapata kinga kamili kwa wakati sahihi.


Amesema ratiba za chanjo zimeandaliwa kitaalamu ili kutoa kinga mapema kulingana na umri wa mtoto, hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo zote kwa wakati uliopangwa ili kuepusha madhara ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.


Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Japhet Simeo ambaye pia ni mwenyekiti wa kikao hicho, amesisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti wa huduma za chanjo katika ngazi zote za utoaji huduma za afya. Amesema viongozi wa afya wanapaswa kuhakikisha upatikanaji wa chanjo, ufuatiliaji wa watoto na utoaji wa elimu kwa jamii vinaimarishwa ili kuongeza uelewa na mwitikio wa wananchi.


Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Andrew Mathew, amebainisha kuwa ushirikiano kati ya watoa huduma za afya, viongozi wa serikali za mitaa na jamii ni muhimu katika kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo. 


Ameongeza kuwa juhudi za kuwafikia watoto waliopo maeneo ya pembezoni zinapaswa kupewa kipaumbele ili kufikia lengo la chanjo kwa wote.


Aidha, Afisa wa Chanjo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Bi. Rosalia Arope, amezungumzia umuhimu wa mafunzo hayo katika kuimarisha uwezo wa wasimamizi wa chanjo.


 Amesema mafunzo ya Uongozi wa Kati yanawajengea washiriki ujuzi wa kupanga, kusimamia na kutathmini huduma za chanjo kwa ufanisi zaidi, hali itakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma hizo katika maeneo yao.


Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa chanjo na kuhakikisha watoto wote wanapata huduma stahiki kwa wakati, hivyo kuchangia kupunguza vifo na magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa chanjo nchini.












🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.
Previous Post Next Post