VIJANA ZUZU WAHAMASISHWA KUGEUKIA KILIMO NA FURSA ZA KIUCHUMI

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Zaidi ya vijana 600 wa Kata ya Zuzu, jijini Dodoma, wanatarajiwa kuandika historia mpya ya ushiriki wao katika maendeleo kupitia Kongamano Kubwa la Vijana lililoandaliwa kwa lengo la kuwawezesha kielimu, kiuchumi na kijamii.


Akizungumza katika kongamano hilo, Afisa Tarafa ya Zuzu, Ibrahim Ally Hassan, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Alhaj Jabir Shekimweri, aliwahimiza vijana kuacha dhana potofu kuwa hakuna fursa katika maeneo yao na badala yake wajikite katika kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa taifa.


Alisema ni jambo la kusikitisha kuona vijana wengi wanakimbia kilimo huku mashambani wakibaki wazee na wanawake wachache wakifanya kazi hiyo muhimu. 


“Tunapodharau kilimo tunapoteza fursa kubwa. 

Mashamba yapo, wataalamu wa kilimo wapo, elimu ipo. Vijana mjikite katika kilimo mjikwamue kiuchumi,” alisisitiza.


Akinukuu takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Hassan alisema asilimia 56.3 ya Watanzania ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 64, hali inayoonesha wazi kuwa vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa. 



Alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetambua umuhimu wa kundi hilo kwa kuunda wizara inayoshughulikia masuala ya vijana ili kusikiliza na kutatua changamoto zao.


Pia aliwahimiza vijana kuchangamkia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalum, akibainisha kuwa Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa wanufaika wa mpango huo. 


Alisema fursa hizo zinalenga kuwawezesha vijana kupata mitaji ya biashara na kujikwamua kiuchumi.


Katika hatua nyingine, Afisa Tarafa huyo aliwataka wakazi wa Zuzu kutunza vyakula, hasa katika kipindi ambacho mvua zinatarajiwa kuwa chache. 


Alionya tabia ya baadhi ya wananchi kutumia mahindi kutengeneza pombe badala ya kuhifadhi chakula kwa matumizi ya baadaye. “Njaa ikija tutamlaumu nani? Tuwajibike kutunza chakula,” alisisitiza.



Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Zuzu, Mhe. Jenesta Project Malingo, alisema wazo la kuandaa kongamano hilo limetokana na kutambua changamoto zinazowakabili vijana, hususan ukosefu wa taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo.


“Mimi pia ni kijana na ninaelewa changamoto zao. Nimeona ni muhimu kuwakutanisha wapate elimu ya uzalendo, fursa za kiuchumi na maadili ili waweze kujitambua na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kata yetu,” alisema.


Alibainisha kuwa licha ya Zuzu kuwa pembezoni mwa mji, ipo katika nafasi ya kipekee kunufaika na miradi mikubwa ya kimkakati kama Reli ya Kisasa (SGR) na Barabara ya Mzunguko wa Nje (Ring Road), ambayo imefungua fursa mbalimbali za ajira na biashara kwa vijana.


Hata hivyo, alitaja changamoto zinazowakabili vijana kuwa ni pamoja na ukosefu wa ajira, matumizi ya dawa za kulevya na mitaji midogo ya kuanzisha shughuli za kiuchumi. 


Alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha vijana katika sekta ya kilimo, ikiwemo kuwapatia miundombinu ya umwagiliaji kama visima kwa ajili ya bustani, pamoja na kuwawezesha vijana wa sekta ya usafirishaji kupata pikipiki ili kujiongezea kipato.



Sambamba na hilo, Mrakimu Msaidizi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, ASP Crista Kayombo, alitoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na kuwasihi wananchi kushiriki katika nyumba za ibada kama njia mojawapo ya kuimarisha maadili na kupunguza vitendo vya ukatili katika jamii.


Naye mmoja wa vijana walioshiriki kongamano hilo, Enyasi Lazaro, alisema elimu waliyoipata imewafumbua macho kuhusu athari za dawa za kulevya, umuhimu wa kutunza fedha na kuchangamkia fursa zilizopo badala ya kubweteka vijiweni wakisubiri ajira.


Kongamano hilo lililofanyika kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni lilijadili mada mbalimbali zikiwemo uzalendo, afya ya akili, fursa za kiuchumi, maadili na mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Kauli mbiu ya kongamano hilo ilikuwa: “VIJANA TUYAJENGE TANZANIA, NI YETU SOTE.”


Kupitia kongamano hilo, Kata ya Zuzu inatarajia kuona kizazi cha vijana chenye mwamko mpya wa uzalendo, uwajibikaji na uthubutu wa kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo binafsi na ya taifa kwa ujumla.



















🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post