UJUMUISHI WA MAKUNDI ANUAI KIPAUMBELE CHA TANZANIA YA KIDIGITALI


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Katika kuhakikisha makundi ya watu wenye mahitaji maalumu hayaachwi nyuma katika maendeleo ya kidigitali, Shirika la Posta Tanzania limepanga kuanza kutumia wataalamu wa lugha ya alama katika vituo vyake ili kurahisisha mawasiliano kati ya watoa huduma na wateja wenye changamoto ya kusikia au kuzungumza.


Hatua hiyo imelenga kuondoa changamoto ya kutokuelewana inayojitokeza pindi watu wenye ulemavu wa kusikia au kuzungumza wanapofika kupata huduma katika vituo vya posta.


Akizungumza na wataalamu wa anuai za jamii kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Meneja wa Shirika la Posta Mkoa wa Dodoma, Dongwe Dongwe, alisema matumizi ya wataalamu wa lugha ya alama yataleta ufanisi na usalama zaidi katika utoaji wa huduma.


Akizungumza Jijini Dodoma leo Jumanne, Februari 3, 2025, Dongwe alisema kwa sasa shirika hilo limekuwa likitumia maandishi kama njia mbadala ya mawasiliano, hali ambayo si salama kwa wateja na wakati mwingine huwanyima uhuru wa kutoa taarifa zao binafsi jambo linaloweza kukwamisha upatikanaji wa baadhi ya huduma.




“Tumewahi kuwa na mteja mwenye changamoto ya kusikia, tulilazimika kuwasiliana kwa kuandika ili kumpatia huduma aliyokuwa anahitaji. Njia hii ina mapungufu mengi, hivyo tumepanga kuimarisha matumizi ya lugha ya alama ili kuwahudumia wateja hawa kwa ufanisi zaidi,” amesema Dongwe.


Ameongeza kuwa, kabla ya kuanza rasmi kwa mpango huo, shirika litatoa mafunzo kwa watumishi wake kuhusu namna bora ya kuwahudumia watu kutoka makundi maalumu yakiwemo watu wenye ulemavu, watoto, wazee na wanawake.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Anuai za Jamii kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mwanaamani Mtoro, alisema Serikali imepanga kufikisha huduma za kidigitali kwa watoto ili kuwajengea uwezo wa matumizi sahihi ya teknolojia wakiwa katika umri mdogo.


Mwanaamani alisema mpango huo unalenga kuwalinda watoto dhidi ya matumizi mabaya ya teknolojia pamoja na kuwajengea uelewa na stadi zitakazowawezesha kunufaika na fursa za kidigitali kwa maendeleo yao binafsi na ya Taifa kwa ujumla.


Amesema huduma hizo zitatolewa kupitia vituo vya utoaji huduma jumuishi vilivyopo chini ya Shirika la Posta pamoja na taasisi za elimu, kwa kuweka mazingira wezeshi yakiwemo vifaa vya kiteknolojia na wataalamu waliobobea.


“Serikali imepanga kuwafikia watoto kwa kuwapatia elimu ya matumizi sahihi ya teknolojia kuanzia wakiwa wadogo, hatua itakayowalinda dhidi ya athari za matumizi mabaya ya teknolojia na kuwajengea msingi imara wa maendeleo ya Taifa letu,” amesema Mwanaamani.



Aidha, Mshauri Muelekezi wa Mradi wa Tanzania ya Kidigitali kwa Makundi Anuai na Ujumuishaji wa Makundi Maalumu katika Mapinduzi ya Kidigitali Tanzania, Caroline Ndosi, alisema kuwa baada ya kutembelea Kituo cha Huduma Jumuishi kilichopo jijini Dodoma, wamejiridhisha kuwa viwango na vigezo vilivyowekwa katika kituo hicho vimezingatia mahitaji ya makundi maalumu na makundi anuai yanayohitaji ujumuishaji katika utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidigitali.


Carloline alisema kuwa serikali inaendelea kutoa wito kwa jamii kutambua na kunufaika na miradi ya aina hiyo, huku ikiendelea kuchukua hatua za makusudi kupitia Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha nchi inafikia mapinduzi ya kidigitali yanayotarajiwa. 


Alisema lengo kuu ni kujenga uchumi wa kidigitali ulio imara na jumuishi unaowagusa wananchi wa makundi mbalimbali wakiwemo vijana, wanawake, watu wenye ulemavu, wazee pamoja na wanaoishi katika mazingira hatarishi.












🚨Full Viddeo Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post