SERIKALI YAZITAKA SEKTA YA FEDHA KUSUKUMA AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA


Na Carlos Claudio,Dodoma📍


Serikali imezitaka taasisi za kifedha nchini kushirikiana na sekta binafsi kuanzisha huduma na bidhaa za kifedha zitakazowezesha ajenda ya nishati safi ya kupikia kusambaa kwa kasi zaidi, hususan kwa kuwawezesha wajasiriamali wadogo katika maeneo ya pembezoni na vijijini pamoja na wabunifu wa teknolojia za nishati hiyo.


Wito huo umetolewa tarehe 4 Februari, 2026 na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, alipomwakilisha Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, katika uzinduzi wa Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia uliofanyika katika Shule ya Sekondari Bunge Wasichana, mkoani Dodoma.


Akizungumza katika uzinduzi huo, Mhe. Makamba alisema Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambapo matumizi yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 23.2 mwaka 2025. Hata hivyo, alisema bado takribani asilimia 77 ya kaya nchini zinatumia nishati isiyo safi ya kupikia.


“Napenda kutoa wito kwa sekta binafsi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kusukuma ajenda hii kwa kuhakikisha upatikanaji wa nishati mbalimbali safi za kupikia unawafikia wananchi walioko maeneo ya pembezoni na vijijini,” alisema Mhe. Salome.



Aidha, aliwataka wasambazaji wa gesi ya kupikia kuongeza vituo vya usambazaji na ujazaji wa mitungi ili kurahisisha upatikanaji wa gesi kwa wananchi wengi zaidi, pamoja na kuwataka wabunifu na vijana walioko vyuoni kufanya tafiti na kubuni teknolojia zitakazosaidia kueneza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.


Kuhusu mradi aliouzindua, Mhe. Makamba alisema ni utekelezaji wa agizo la Serikali linalozitaka taasisi zote zinazolisha watu zaidi ya 100 kutumia nishati safi ya kupikia, hatua inayolenga kulinda afya za binadamu na kutunza mazingira.


Aliongeza kuwa mfumo huo wa nishati safi utawezesha chakula kupikwa kwa usafi, haraka, kwa ufanisi na kwa gharama nafuu, huku ukiondoa madhara ya moshi kwa wapishi na wanafunzi pamoja na kulinda mazingira.


Mhe. Makamba alisema uzinduzi wa mradi huo ni sehemu ya juhudi za kitaifa zinazoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. Alisema hadi sasa taasisi 1,136 zinazolisha zaidi ya watu 100 kwa siku tayari zimehamia katika matumizi ya nishati safi.


Katika hafla hiyo, Naibu Waziri alizindua pia Klabu ya Nishati Safi ya Kupikia (Clean Cooking School Club) katika Shule ya Sekondari Bunge Wasichana, klabu ya kwanza ya aina yake nchini. Alisema klabu hiyo itakuwa mfano wa kuigwa na shule nyingine nchini katika kueneza elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.


Wanafunzi watakaojiunga na klabu hiyo watakuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia na kushirikiana na Wizara ya Nishati pamoja na wadau wengine kutoa elimu katika jamii na kubuni teknolojia rafiki kwa afya na mazingira.


Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bunge Wasichana, Richard Msana, alisema shule hiyo yenye wanafunzi 555 imefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za nishati ya kupikia baada ya kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia katika matumizi ya gesi.



Alisema kati ya Julai 2020 hadi Mei 2022, shule ilikuwa ikitumia takribani shilingi milioni 10.5 kila baada ya miezi mitatu kununua kuni. Baada ya kutumia mkaa mbadala gharama zilishuka hadi shilingi milioni 2.7, na kwa sasa kupitia matumizi ya gesi, shule hutumia wastani wa shilingi milioni 1.3 kwa mwezi, kiwango ambacho ni nafuu zaidi kiuchumi.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweru, aliipongeza Serikali kwa kuiteua shule hiyo kuwa miongoni mwa walengwa wa miradi ya maendeleo, akisema ni shule vinara wilayani humo.


Naye Mwakilishi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mbunge wa Jimbo la Mbinga, Mhe. Jonas Mbunda, alisema Serikali ya Awamu ya Sita imetoa fedha nyingi kuhakikisha nishati safi ya kupikia inawafikia wananchi wengi zaidi, huku Kamati ikiridhishwa na utekelezaji wa miradi ya nishati nchini.


Akitoa taarifa ya mradi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, James Mataragio, alisema tafiti zinaonesha zaidi ya watu milioni mbili hufariki kila mwaka duniani kutokana na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia, huku wanawake na watoto wakiwa waathirika wakubwa zaidi nchini Tanzania.


Alisema utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia utasaidia kulinda mazingira, kuboresha afya za wananchi na kuongeza tija katika taasisi za elimu na jamii kwa ujumla.





🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post