NIC KUHAKIKISHA ULINZI WA MALI SOKO LA KARIAKOO



Na Carlos Claudio, Dar Es Salaam.📍


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema kuwa hakuna mfanyabiashara atakayeruhusiwa kuanza au kuendelea na biashara ndani ya jengo la Soko la Kariakoo mpaka jengo hilo litakapolipiwa bima kwa mujibu wa taratibu na sheria za bima nchini Tanzania.


Akizungumza mara baada ya hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ushirikiano kati ya Shirika la Masoko la Kariakoo na Shirika la Bima la Taifa (NIC), Chalamila alisema hatua hiyo inalenga kulinda mali za umma na za wafanyabiashara dhidi ya majanga yasiyotabirika.



“Hatutaruhusu mfanyabiashara yeyote kuendelea na shughuli zake hadi pale jengo litakapokuwa limewekewa bima. Endapo madhara yatatokea, basi bima itaweza kufidia kwa kufuata sheria na kanuni za bima nchini,” alisema Chalamila.


Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Soko la Kariakoo, Ashraph Abdulkarim, alisema soko hilo linaelekea kuwa la kisasa zaidi kufuatia maboresho makubwa ya miundombinu na upangaji wa maeneo ya bidhaa.


Alikumbusha kuwa tukio la moto lililotokea awali liliacha huzuni kubwa na hasara kwa wafanyabiashara wengi, huku jengo likiwa halina bima. Kutokana na fundisho hilo, uongozi wa soko umeona umuhimu wa kusaini mkataba huo wa ushirikiano na NIC ili kuhakikisha mali zote zinalindwa ipasavyo.


“Tukio lile lilituumiza sana. Wafanyabiashara wengi walipoteza mali zao zote. Sasa tumedhamiria kuhakikisha mali ya umma na mali za wafanyabiashara zinalindwa kwa bima,” alisema Abdulkarim.



Baadhi ya wafanyabiashara walioshuhudia janga hilo wameeleza matumaini yao juu ya hatua mpya zilizochukuliwa. Emmanuel Msibe, mfanyabiashara katika soko hilo, alisema walipoteza kila kitu na kulazimika kuanza upya bila msaada wa bima.


“Ni kweli tulipoteza mali zote. Ilikuwa ni safari ngumu sana kuanza tena biashara, lakini tunaamini sasa tupo salama zaidi,” alisema Msibe.


Naye mfanyabiashara Mwajuma Saidi alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi za kuliimarisha soko hilo na kulifanya kuwa la kisasa.


“Soko limeboreshwa sana. Zamani kulikuwa na soko dogo la chini, lakini sasa tuna jengo kubwa la ghorofa lenye hadhi na mazingira bora ya biashara,” alisema Mwajuma.


Hatua ya kuweka bima kwa jengo la Soko la Kariakoo inatajwa kuwa ni mwanzo wa enzi mpya ya usalama wa biashara katika moja ya masoko makubwa na yenye shughuli nyingi zaidi nchini, likiwa ni kitovu muhimu cha uchumi wa Jiji la Dar es Salaam.







🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post