Na Carlos Claudio, DOdoma.📍
Kata ya Zuzu inatarajia kuandika historia mpya ya ushiriki wa vijana kupitia Kongamano Kubwa la Vijana litakalowakutanisha zaidi ya vijana 600 kutoka maeneo mbalimbali ya kata hiyo. Kongamano hili limeandaliwa kwa lengo la kuwawezesha vijana kielimu, kiuchumi na kijamii, sambamba na kuwapa jukwaa la kutoa maoni na changamoto zao.
Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Zuzu, mhe. Jenesta Project Malingo, kongamano hili ni sehemu ya juhudi za makusudi za kuimarisha nafasi ya vijana katika ujenzi wa jamii na taifa kwa ujumla. Tukio hilo litafanyika kuanzia saa 03:00 asubuhi kamili hadi saa 10:00 jioni kamili, likiwa na ajenda mbalimbali zinazogusa maisha halisi ya vijana.
Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa ni pamoja na uzalendo na nafasi ya vijana katika kulinda amani ya nchi, fursa za kiuchumi kwa vijana, elimu ya afya ya akili, pamoja na elimu kuhusu ukatili wa kijinsia. Aidha, kutakuwa na mjadala kuhusu umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, athari za madawa ya kulevya, na maadili kwa vijana katika jamii ya leo.
Kongamano hili halitakuwa tu jukwaa la kusikiliza mada, bali pia nafasi ya wazi kwa vijana kushiriki kikamilifu kwa kutoa maoni, mapendekezo na kueleza changamoto zinazowakabili katika harakati zao za kujiletea maendeleo.
Kauli mbiu ya kongamano hili ni: “VIJANA TUYAJENGE TANZANIA NI YETU SOTE.” Kauli hii inalenga kuhamasisha uwajibikaji, mshikamano na uzalendo miongoni mwa vijana, wakitambua kuwa mustakabali wa taifa uko mikononi mwao.
Vijana wote wa Kata ya Zuzu wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kongamano hili muhimu, ambalo linatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko chanya na maendeleo endelevu kwa vijana na jamii kwa ujumla.
🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

