IAA YAJIPANGA KUWAANDAA VIJANA KUJIAJIRI, YAIMARISHA ELIMU YA FEDHA


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍

Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kimeendelea kujizatiti katika kuwaandaa vijana kujiajiri kwa kuwapatia elimu ya fedha, ujuzi wa biashara na mbinu za kubadili maarifa yao kuwa fursa halisi za ajira.


Akizungumza Februari 20, 2026 jijini Dodoma, Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eliamani Sedoyeka, alisema changamoto kubwa inayowakabili vijana siyo ukosefu wa elimu au ujuzi wa kitaaluma, bali ni kushindwa kuugeuza ujuzi huo kuwa shughuli za kiuchumi zenye tija.


Alifafanua kuwa IAA imeweka mkazo katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuanzisha na kusimamia biashara, ambapo kila mwanafunzi hupatiwa elimu ya fedha pamoja na mafunzo ya namna ya kuandaa mipango ya biashara inayotekelezeka.


Kupitia kituo atamizi cha chuo hicho, vijana hupata fursa ya kukuza mawazo yao ya kibiashara na kuyaendeleza kitaalamu hadi kufikia hatua ya utekelezaji. Aidha, wanafunzi hupewa mafunzo ya nidhamu ya matumizi ya fedha na mbinu za kupata mitaji kupitia maandiko ya biashara.


Prof. Sedoyeka alibainisha kuwa chuo kinahamasisha vijana kuanza na rasilimali walizonazo, akitoa mfano wa baadhi ya wanafunzi wanaoanza na biashara ndogo kama kuuza uji, ambazo hukua na kuwa miradi mikubwa inayoweza hata kuajiri wengine.


Katika kuimarisha ajira kwa vijana, chuo hicho pia kimeanzisha mtaala mpya wa uhasibu na kodi unaolenga kumwezesha mhitimu kujiajiri. Wahitimu wanatarajiwa kusaidia biashara ndogo na za kati katika kuandaa hesabu, kusimamia taarifa za fedha na kutimiza mahitaji ya kikodi.


Aliongeza kuwa mtaala wa kimataifa wa uhasibu unawawezesha wanafunzi kupata ujuzi unaokubalika kimataifa, hivyo kuwapa nafasi ya kuingia katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.


Kwa sasa, IAA ina jumla ya wanafunzi 20,993 katika kampasi zake mbalimbali, huku asilimia kubwa wakiwa vijana wenye umri wa wastani wa miaka 20. Hata hivyo, takribani wanafunzi 1,000 hawapo katika hali ya masomo endelevu kutokana na changamoto mbalimbali.


Katika hatua nyingine, Prof. Sedoyeka alisema chuo kimenufaika na mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ambapo kimepokea zaidi ya shilingi bilioni 48 kwa ajili ya kuboresha miundombinu, mitaala na matumizi ya teknolojia.


Fedha hizo zimeelekezwa katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya kufundishia, mapitio ya mitaala ili iendane na mahitaji ya soko la ajira, pamoja na kuimarisha TEHAMA na kuwajengea uwezo watumishi wa chuo.


Aidha, chuo kimeunda Kamati ya Ushauri ya Kisekta ili kuimarisha uhusiano kati ya mafunzo na mahitaji halisi ya soko la ajira, sambamba na kusaini mikataba 23 ya ushirikiano na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.


Katika maboresho ya mitaala, jumla ya mitaala 15 imefanyiwa mapitio, huku mingine mipya ikiendelea kuandaliwa katika fani mbalimbali zikiwemo uhandisi, usindikaji wa vyakula, na usimamizi wa biashara katika sekta za misitu, maziwa na uvuvi.


Kupitia mradi huo, wahadhiri 115 wanaendelea na masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) ndani na nje ya nchi, hatua inayolenga kuongeza ubora wa ufundishaji na utafiti chuoni hapo.


Prof. Sedoyeka alisisitiza kuwa juhudi hizo zinalenga kuzalisha wahitimu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kujitegemea, huku wakichangia moja kwa moja katika maendeleo ya uchumi wa taifa.


“Vijana wana ujuzi, lakini changamoto iliyopo ni namna ya kuugeuza ujuzi huo kuwa ajira na fursa za kuwaajiri wengine,” alisisitiza.



🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post