Wataalamu wanaohusika na zoezi la ukusanyaji wa sampuli za udongo kwa ajili ya upimaji wa afya ya udongo nchini, wamefanya kikao kazi kinacholenga kujadili na kutoa elimu ya namna bora ya ukusanyaji wa sampuli za udongo, kwa ajili ya upatikanaji wa ramani ya Afya ya udongo kidigitali pamoja na usimamizi sahihi wa ardhi ya kilimo.
Kikao kazi hicho kimefanyika tarehe 6 Januari 2026 mkoani Morogoro na kuhusisha wataalamu kutoka Wizara ya kilimo, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ( TARI) Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), Bodi ya Mkonge, Chuo cha Sukari cha Taifa, Vyuo vya Kilimo ( MATI), Maafisa kilimo, wataalamu kutoka Chuo cha Kilimo cha Sokoine ( SUA), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) pamoja na wahitimu kutoka katika vyuo mbalimbali nchini.
Akiwasilisha mada katika kikao kazi hicho Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kilimo
( DLUP) kutoka Wizara ya Kilimo Mha. Juma Mdeke, amewataka washiriki wa zoezi hilo kuhakikisha wanajenga timu imara kwa kuzingatia misingi ya mawasiliano bora, uhusiano wa karibu, kujiamini pamoja na kuwa tayari kutoa na kupokea mrejesho.
" Ni muhimu kuhakisha mawasiliano yetu katika timu yanakua mazuri zaidi ili kurahisisha utendaji kazi wetu katika timu kwasababu iwapo yatakosekana mawasiliano mazuri baina ya mtu na mtu ndani ya timu basi kazi hii itakwama, na mawasiliano haya yanapokelewa kutokana na uhusiano mzuri iwapo mtakosa uhusiano mzuri basi mawasiliano hayo yanaweza kupokelewa tofauti na ulivyokusudia", amesema mhandisi Mdeke
Amewataka kuzingatia misingi muhimu ya kuaminiana, kutatua migogoro, uwajibikaji pamoja na kujikita katika kufikia lengo husika, akihitimisha kwa kusema timu si kuwa pamoja tu bali ni kuaminiana.
Naye Afisa Kilimo Mkuu na Afisa Kiungo wa Mradi wa TFSRP katika kiashiria namba 7 Bw. Ntirankiza Misibo, amesema zoezi hili litawezesha upatikanaji wa ramani ya afya ya udongo kidigitali, itakayotoa taarifa sahihi kuhusu aina ya udongo, zao linalostahili kulimwa katika udongo huo, matumizi sahihi ya mbolea pamoja na matumizi sahihi ya zana za kilimo.
Upatikanaji wa ramani hiyo utawawezesha wafanya maamuzi na watunga sera kuweka mipango mizuri inayohusu Sekta ya kilimo kupitia taarifa muhimu zitakazopatikana katika ramani hiyo.
"Zoezi hili litarahisisha upatikanaji wa ramani ya afya ya kilimo kidigitali itakayomuwezesha mkulima kuzalisha kwa tija kupitia taarifa za msingi zitakazokua katika ramani hiyo kuhusu aina ya zao lipi alime, atumie mbolea ipi na zana zipi za kilimo katika uzalishaji, vile vile kwa watunga Sera katika upangaji wa mikakati na raasilimali za kilimo", amesema Bw. Misibo.
Hatua hii ni utekelezaji wa Mikakati ya Wizara ya Kilimo kupitia Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) kiashiria namba 7, zoezi ambalo ni uhaulishaji wa upimaji wa afya ya udongo wa mwaka 1984 uliofanyika kwa mizani ya 1:2000000, upimaji wa sasa unafanyika kwa mizani ya 1:50000 ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa za kina nchini kuhusu afya ya udongo ukilinganisha na mizani iliyotumika katika upimaji wa hapo awali.
Jumla ya mikoa 13 nchini ambayo ni Ruvuma, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Singida, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Geita, Mara, Kigoma na Kagera imefikiwa na zoezi la upimaji wa afya ya udongo na hivi sasa wataalamu wanaendelea na ukusanyaji wa sampuli za udongo katika mikoa ya Tabora, Morogoro, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara
Wataalamu hao pia wamejifunza namna ya kuchukua sampuli hizo na kupata elimu zaidi kuhusu ramani za msingi pamoja na Mfumo wa Taarifa za Kijiografia (GIS)



