Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amewataka wadau wote wanaosimamia ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo mwezi Mei mwaka huu.
Akizungumza jijini Dodoma Januari 14, 2026 wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo, Prof. Mbarawa alisema kuwa mradi umefikia hatua ya ukamilishaji (finishing) ambayo inahitaji umakini wa hali ya juu, matumizi sahihi ya fedha na ubora wa vifaa vinavyotumika ili kuendana na mahitaji ya uendeshaji wa uwanja wa ndege wa kimataifa.
Alisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu baina ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Idara ya Zimamoto na Uhamiaji ni muhimu ili mifumo na vifaa vya uendeshaji visomane na kurahisisha utendaji wa shughuli za uwanja huo mara baada ya kufunguliwa rasmi.
“Katika ukaguzi huu, Waziri ametupatia maelekezo mbalimbali, yakiwemo maelekezo makuu matatu yanayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya TANROADS, Wizara ya Uchukuzi, TAA na TCAA, hasa katika kipindi hiki cha kukamilisha kazi za mwisho za finishing,” alisema Eng. Amani.
Aliongeza kuwa TANROADS itaendelea kusimamia kwa karibu kazi zote muhimu ikiwemo ufungaji wa lifti, mifumo ya uendeshaji katika majengo mawili ya abiria pamoja na jengo la mnara wa kuongozea ndege (control tower), ili kuhakikisha kazi zinafanyika kwa thamani ya fedha na ubora unaotakiwa.
Naye Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, Clemence Mbaruck, alisema kuwa TAA kama mtumiaji mkuu wa uwanja huo imepokea maelekezo ya Waziri wa Uchukuzi na iko tayari kuyatekeleza kikamilifu.
Alisema mamlaka hiyo imeweka wataalamu katika eneo la mradi kwa ajili ya kufuatilia na kusimamia ujenzi ili kuhakikisha vifaa vinavyowekwa pamoja na kazi zote zinazotekelezwa zinakidhi viwango na masharti ya mkataba.
Mbaruck aliongeza kuwa tayari watumishi 170 wa TAA wameshahamishiwa Dodoma kwa ajili ya kuanza kazi katika uwanja huo mara baada ya kufunguliwa rasmi.
Mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 370 na unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa wakazi wa Dodoma na Taifa kwa ujumla, kwa kuruhusu ndege za aina mbalimbali za ndani na nje ya nchi kutua na kuondoka katika uwanja huo.
🚨Full Video Inapatikana katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.











