Serikali imesema itahakikisha kila mwananchi mwenye aridhi anapata hati miliki, na kuwaasa watendaji kuacha urasimu na kumsaidia Rais kuleta furaha kwa wananchi wa Tanzania.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye Kliniki Maalum ya Ardhi inayoendelea katika Ofisi za Ardhi Mkoa wa Dodoma leo tarehe 28 Januari, 2026 Naibu waziri wa Aridhi Mheshimiwa Caspal Muya Mmuya (MB) amesema, upo umuhimu wa kuhakikisha wananchi waliokamilisha taratibu za kumilikishwa wanapata hati zao kwa kuwa wapo waliofuatilia kwa muda mrefu.
"Nitasimamia kuhakikisha kila mwananchi mwenye uhalali wa kumiliki Ardhi anapata hati yake kwa wakati” amesema Naibu Waziri Mmuya.
Amesema Ili kutoa huduma bora, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewataka wataalamu wa Sekta ya Ardhi nchini kuhakikisha wanatoa elimu ya matumizi bora ya ardhi pamoja na jinsi ya kupata hatimiliki za ardhi, hatua aliyoieleza itasaidia kuepusha ujenzi holela unaoenda kinyume na matumizi yaliyopangwa.
Mheshimiwa Caspal Mmuya amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kusimamia haki ya umiliki wa ardhi kwa vitendo na kuhakikisha wamiliki wa ardhi wanapata hati zao.
Ameeleza kuwa, Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawahakikishia wananchi kuendelea kupata huduma za hati katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameongeza kuwa, wizara hiyo chini ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo imeweka mkakati wa siku 14 kuhakikisha kila mwananchi wa Jiji la Dodoma aliyekidhi vigezo vya kupata hati milki ya ardhi anapata hati yake hatua aliyoieleza kuwa, itasaidia kurahisisha huduma na kulinda haki za wananchi.
Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga amesema, wamiliki wa ardhi waliokamilisha taratibu za umiliki wapewe Hatimiliki zao na hawahitaji maneno mengi., na kuwataka watumishi kuondoa urasimu katika kufanikisha zoezi hilo.
Mhandisi Sanga amesisitiza kuwa, ni marufuku kwa mtumishi wa sekta ya ardhi anayefutwa na mwanachi mwenye shida kumwambia aende kwa mtu mwingine kupata huduma na kueleza kuwa, atasimamia msimamo huo kwa kuwa mwananchi anachohitaji ni huduma.
Katika siku ya kwanza ya zoezi hilo, tayari zaidi ya Hatimiliki 20 zimetolewa na zaidi ya 100 zipo katika hatua za mwisho za kukamilika kwake.
🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.






