MHESHIMIWA WAZIRI MKUU KUZINDUA MKAKATI WA TAIFA WA ZANA ZA KILIMO AWAMU YA PILI.

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), anatarajiwa kuzindua rasmi Mkakati wa Taifa wa Zana za Kilimo Awamu ya Pili (National Mechanization Strategy Phase Two 2026–2035), ambao utakuwa mwongozo mkuu wa kuongeza tija katika sekta ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa.


Hayo yamesemwa leo, Januari 30, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), wakati akizungumza na waandishi wa habari. 


Amesema kuwa uzinduzi wa mkakati huo utafanyika sambamba na Mkutano wa Afrika kuhusu Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo (Africa Conference on Sustainable Agricultural Mechanization – ACSAM), unaotarajiwa kufanyika kuanzia Februari 3 hadi 6, 2026 katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri Mkuu atakuwa mgeni rasmi.



Mhe. Chongolo amesema mkutano huo ni matokeo ya ushirikiano kati ya Wizara ya Kilimo na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), ukiwa na lengo la kutoa jukwaa kwa wadau wa sekta ya kilimo kubadilishana uzoefu, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, pamoja na kuharakisha matumizi ya zana za kisasa za kilimo kwa ajili ya mageuzi endelevu ya kilimo nchini Tanzania na Barani Afrika kwa ujumla.


Ameeleza kuwa Mkakati wa Taifa wa Zana za Kilimo Awamu ya Pili unalenga kuimarisha matumizi, utengenezaji, uendelezaji, uhamasishaji, usimamizi na uratibu endelevu wa teknolojia zinazorahisisha kazi, kuokoa muda na kuongeza ufanisi katika mnyororo mzima wa uzalishaji na uongezaji wa thamani wa mazao ya kilimo.


Kwa mujibu wa Waziri huyo, mkutano wa ACSAM unatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya washiriki 1,500, wakiwemo Mawaziri wa Kilimo kutoka nchi mbalimbali Barani Afrika, washirika wa maendeleo, viongozi waandamizi wa FAO wa kikanda na kimataifa, wakuu wa taasisi za umma, wawakilishi wa sekta binafsi, wataalamu wa kilimo pamoja na wakulima kutoka nchi mbalimbali za Afrika.


“Mkutano huu ni fursa muhimu kwa Tanzania kuonesha dhamira yake katika kuendeleza kilimo cha kisasa na chenye tija, sambamba na kujifunza kutoka kwa nchi nyingine kuhusu matumizi endelevu ya zana na teknolojia za kilimo,” amesema Mhe. Chongolo.


Wizara ya Kilimo imetoa wito kwa wadau wote wa sekta ya kilimo, taasisi za umma na binafsi pamoja na wananchi kwa ujumla kufuatilia na kushiriki kikamilifu katika mkutano huo, ambao ni muhimu kwa maendeleo ya kilimo na ustawi wa wakulima nchini na Barani Afrika.




🚨Full VIDEO Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post