Na Edward Winchislaus,Dodoma.📍
Serikali imeendelea kuonesha dhamira thabiti ya kuwawezesha wanawake kiuchumi kama njia ya kutatua changamoto za kijamii na kukuza maendeleo jumuishi.
Waziri wa Madini na Mbunge wa Mtumba, Mhe. Anthony Mavunde, amebainisha hayo Januari 12,2026 jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa wanawake wa Taasisi ya Wanawake na Samia waliomaliza mafunzo ya ufundi stadi katika Chuo cha VETA Dodoma.
Akihutubia wahitimu hao, Mavunde amesema kuwa falsafa ya serikali ni kuwekeza kwa mwanamke kwa sababu matokeo yake huonekana moja kwa moja katika familia na jamii kwa ujumla huku akisema kuwa ndani ya muda mfupi tangu wanawake hao walipoanza mafunzo, tayari kuna dalili za mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, hali inayoonesha ufanisi wa mpango huo ambapo amesisitiza kuwa Dodoma sasa imekua kwa kasi na imejaa fursa nyingi za kiuchumi zinazohitaji ushiriki mkubwa wa wanawake.
Katika hatua nyingine, Mavunde ametangaza mpango wa kuanzisha Kijiji cha Wanawake na Samia kitakachokusanya shughuli zote za kiuchumi za wanawake hao katika eneo moja la kati ya jiji la Dodoma lenye mzunguko mkubwa wa watu. Amesema atafanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma ili kuhakikisha eneo hilo linapatikana, huku akiahidi kusaidia gharama za pango kwa shughuli za awali wakati wakisubiri eneo la kudumu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Samia Dodoma na Tanzania nzima Bi.Fatuma Madidi amesema mafunzo hayo yalitokana na ushirikiano kati ya mwasisi wa taasisi hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, na uongozi wa VETA. Ambapo amesema zaidi ya wanawake 600 walishiriki katika awamu ya kwanza wakipata mafunzo ya fani mbalimbali ikiwemo mapishi, ushonaji, mapambo na usafi kwa viwango vya juu vya ujuzi na weledi.
“Mafunzo haya yalitolewa kwa kuzingatia umahiri wa kila fani bila kuweka kikomo cha muda. Hawa si wanawake wa kawaida, bali ni wataalamu waliopo tayari kuingia sokoni na kujiajiri,” amesema mwenyekiti huyo.
Hata hivyo ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kudhamini mafunzo hayo, na akampongeza Mhe. Mavunde kwa kuwa mlezi wa wanawake hao na kukabidhi vitendea kazi vya awamu ya kwanza vyenye thamani ya shilingi milioni 10, hatua inayotarajiwa kuongeza ajira na kipato kwa wanawake wa Dodoma.






