Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
MKUU wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Mayeka S. Mayeka, ametoa onyo kali kwa wananchi wanaovamia na kuendesha shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo, ujenzi na shughuli nyinginezo katika chanzo cha maji cha Mbuyuni kilichopo Kibaigwa, akisisitiza kuwa ni marufuku kabisa kufanya shughuli zozote katika vyanzo vya maji.
Akizungumza leo Januari 29, 2026 wakati wa uzinduzi wa zoezi la upandaji miti katika chanzo hicho cha maji, Mhe. Mayeka amesema suala la vyanzo vya maji halina siasa, hivyo Serikali haitasita kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wote watakaobainika kukiuka sheria kwa kulima, kujenga au kuharibu mazingira ya eneo hilo.
Amesema upungufu wa maji ni tishio la kiusalama na maendeleo ya jamii, hivyo ulinzi wa vyanzo vya maji ni jambo nyeti linalohitaji ushirikiano wa Serikali na wananchi wote.
Amehimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika upandaji miti na utunzaji wa mazingira ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji safi na salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Mhe. Mayeka ameeleza kuwa idadi ya watu katika mji wa Kibaigwa inaongezeka kwa kasi, hali inayosababisha ongezeko la mahitaji ya maji.
Ameonya kuwa uharibifu wa chanzo cha maji ni sawa na kuwanyima wananchi haki yao ya msingi ya kupata huduma ya maji, akisisitiza kuwa chanzo cha maji ni mali ya wananchi wote na si cha DUWASA pekee, ambao ni wasimamizi wa rasilimali hiyo.
Ameongeza kuwa uharibifu wa mazingira haukopeshi kwani madhara yake hujitokeza haraka, hivyo amewataka wananchi waliovamia eneo la chanzo cha maji, wakiwemo waliolima au kujenga kinyume cha sheria, kuondoka mara moja bila kusubiri hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya amesema jumla ya wananchi 24 tayari wamelipwa fidia ili kupisha eneo la chanzo cha maji, huku akitoa onyo kwa wale wanaoendelea kulima au kufanya shughuli nyingine karibu na chanzo hicho kuacha mara moja, kwani ni kinyume cha sheria.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa DUWASA, Eng. Aron Joseph, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo Rahel Muhando amesema DUWASA inaendelea kutambua mchango mkubwa wa mazingira katika uhifadhi na uendelevu wa vyanzo vya maji.
Amesema upandaji miti ni moja ya njia muhimu za kulinda vyanzo vya maji ili viendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.
Amehimiza wananchi kuendeleza utamaduni wa kupanda na kutunza miti hususan katika maeneo yanayozunguka vyanzo vya maji, akisisitiza kuwa uzalendo wa kweli unaanza na utunzaji wa mazingira.
“Uzalendo wa kweli ni kutunza mazingira. Kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki katika kulinda vyanzo vya maji kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla,” imeelezwa katika kauli ya DUWASA.
Zoezi hilo la upandaji miti ni sehemu ya mikakati ya DUWASA kwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya ya Kongwa, yenye lengo la kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama sambamba na kuimarisha uhifadhi wa mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.
🚨Full Video Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.









