Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Viongozi wa dini na serikali nchini wametakiwa kusimamia haki, usawa na kuendeleza maombi kwa ajili ya taifa ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kubaki katika amani, umoja na baraka za Mungu.
Wito huo umetolewa leo Desemba 27, 2025 jijini Dodoma na Askofu Dkt. Mussa Mlawi, Raisi wa Tanzania Pastors Association (TPA), wakati wa ibada maalum ya kuliombea taifa la Tanzania pamoja na kuwatunuku wahitimu wa mahafali ya 14 ya Chuo cha Africa Bible College International Tanzania (ABCI-T).
Askofu Dkt. Mlawi alisema licha ya kasoro na uzembe uliowahi kujitokeza hapo nyuma kwa upande wa viongozi wa dini na serikali, bado taifa lina nafasi ya kurejea kwa Mungu kwa toba ya kweli ili liendelee kupokea baraka na ulinzi wake.
Alisisitiza kuwa baraka za taifa hazitoki kwa wanadamu bali zinatoka kwa Mungu, hivyo ni wajibu wa taifa zima kumtanguliza Mungu katika kila jambo.
“Taifa letu linahitaji kuungana, kuacha matabaka na migawanyiko ya makundi, tuwe na sauti moja, lugha moja na kauli moja ya kulinda amani ya nchi yetu. Mungu akikasirika, kurejesha amani huwa ni jambo gumu,” alisema Askofu Mlawi.
Aliongeza kuwa mivutano ya kauli na misimamo tofauti baina ya makundi mbalimbali haiwezi kulijenga taifa, bali kinachohitajika ni taifa kurejea kwa Mungu, kutubu na viongozi wa dini kujitathmini ni wapi walimkosea Mungu na kurekebisha njia zao.
Katika maombi hayo, viongozi wa dini waliomba Mungu kuliepusha taifa na majaribu yanayoweza kuisukuma nchi kwenye machafuko, huku wakisisitiza kuwa maombi hayo yamewakilisha kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa zima.
Askofu Mlawi alitoa wito kwa viongozi wote wa kiroho na kidini nchini kuendeleza maombi kama hayo kila mahali ili neema ya Mungu iendelee kutiririka juu ya Tanzania.
Pia aliwataka Watanzania kuendelea kuwaombea viongozi wa serikali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili waendelee kuwa na maono mapana ya kuwatumikia wananchi, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi pekee waliyonayo Watanzania.
Ibada hiyo ilihitimishwa kwa maombi ya pamoja ya kuliweka taifa mikononi mwa Mungu, huku viongozi wakisisitiza kuwa amani, umoja, mshikamano na upendo ni nguzo muhimu zitakazoiwezesha Tanzania kuendelea kuwa kisiwa cha amani na mahali salama pa kuishi.
🚨Full Video Inapatikana Katika Youtube Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.


















