PPRA YAWAJENGEA UWEZO WANAHABARI DODOMA KUHUSU UNUNUZI WA UMMA


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍

Meneja Mafunzo wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Gilbert Kamnde, leo Desemba 23, 2025, amewafafanulia waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma kuhusu utendaji kazi wa mamlaka hiyo katika semina iliyofanyika kwenye ofisi za Ununuzi wa Umma mkoani Dodoma.

Akizungumza katika semina hiyo ya kuwajengea uwezo wanahabari, Kamnde amesema PPRA inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma iliyopitishwa na Bunge mwaka 2001 pamoja na kanuni zake mpya za Ununuzi za Serikali (GN Na. 518 za mwaka 2024), sambamba na matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa NeST katika ununuzi wa umma.

Alifafanua kuwa lengo la semina hiyo ni kuwawezesha wanahabari kuuelewa mfumo wa ununuzi wa umma, uwajibikaji na uwazi katika matumizi ya fedha za serikali, ili waweze kuhabarisha umma kwa usahihi.

Katika semina hiyo, wanahabari walielezwa kuwa Serikali inaruhusiwa kununua bidhaa tatu pekee zilizotumika kwa manufaa ya umma ambazo ni ndege, meli na treni, huku bidhaa nyingine zote zinazotumika katika ununuzi wa umma zikitakiwa kuwa mpya.

Kamnde alisisitiza kuwa utekelezaji wa kanuni hizo unalenga kulinda maslahi ya umma, kuongeza thamani ya fedha na kuimarisha uwazi katika manunuzi ya serikali.






🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.
Previous Post Next Post