Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Afisa Habari wa Taasisi ya Maendeleo na Uchumi Organization (UMO), Bakari Kiwingu, amewatakia Watanzania wote heri ya Krismasi na Mwaka Mpya, huku akitumia fursa hiyo kutangaza ujio wa kampeni maalum ya kitaifa kwa vijana itakayojulikana kwa jina la “Kijana ni Fursa na Wewe Umo”, itakayotekelezwa mwaka 2026.
Akizungumza kwa niaba ya Taasisi ya UMO kupitia Idara ya Habari na Mawasiliano Taifa, Kiwingu amesema kampeni hiyo inalenga kuwafikia vijana wa Kitanzania wa kike na wa kiume kote nchini, kuanzia ngazi ya mitaa, wilaya hadi mikoa, kwa lengo la kuwaelimisha na kuwaonesha fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo katika maeneo yao pamoja na fursa zitokanazo na Serikali.
Ameeleza kuwa dhamira kuu ya kampeni hiyo ni kuhakikisha vijana wanatambua, wanatumia na kunufaika ipasavyo na rasilimali zilizopo katika maeneo yao na taifa kwa ujumla, ili kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya nchi.
“Tunaomba ushirikiano kutoka kwa vijana wote Tanzania nzima pale tutakapofika katika mitaa, wilaya na mikoa yao. Lengo letu siyo tu kuzungumza, bali kuonesha kwa vitendo fursa zilizopo katika maeneo yao na namna ya kuzifikia,” amesema Kiwingu.
Ameongeza kuwa UMO inatambua changamoto ya upungufu wa ajira kwa vijana, lakini amesisitiza kuwa vijana hawapaswi kubweteka wala kulalamika, wakati kuna fursa nyingi zinazowazunguka katika mitaa, majiji, mikoa na nchi kwa ujumla.
“Ni muhimu vijana tukazungumza na kueleweshana namna ya kuzifikia fursa hizi ili tuweze kujikwamua kiuchumi. 2026 ni mwaka wetu vijana, ni mwaka wa kuamka, kufanya kazi na kuchangamkia fursa,” amesema.
“Sisi kama sauti ya vijana na taasisi ya maendeleo na uchumi, UMO Tanzania, tunakuja kwenu. Mtupokee. Tunakuuliza kijana: Kijana ni fursa, je na wewe umo?” amehoji.
Kampeni ya “Kijana ni Fursa na Wewe Umo” inatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko ya fikra kwa vijana, ikiwahamasisha kuacha kulalamika na badala yake kuchukua hatua za vitendo katika kujenga maisha yao na taifa kwa ujumla.


