DARAJA LA NZALI LAONDOSHA ADHA YA MAWASILIANO, WANANCHI CHAMWINO WANUFAIKA

 


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Wananchi wa Kijiji cha Nzali, Kata ya Chilonwa wilayani Chamwino mkoani Dodoma, wameishukuru Serikali kwa kuwajengea daraja la kisasa lililoondoa adha ya kukosa mawasiliano kwa miaka mingi, hususan nyakati za mvua ambapo baadhi ya wananchi walikuwa wakisombwa na maji na kushindwa kupata huduma muhimu za kijamii kama afya na elimu.


Shukrani hizo zimetolewa leo Desemba 22, 2025 katika hafla ya makabidhiano ya daraja hilo lenye urefu wa mita 60, ambalo limefikia asilimia 98 ya ukamilishaji na linatarajiwa kukamilika rasmi Desemba 30 mwaka huu.


Wakizungumza kwa niaba ya wananchi, wamesema ujenzi wa daraja hilo ni mkombozi mkubwa kwa kijiji hicho kwani utaondoa kero ya kukatika kwa mawasiliano, kurahisisha usafiri na usafirishaji wa watu na mazao, kuongeza fursa za biashara pamoja na kuimarisha shughuli za kiuchumi.


Wananchi hao wameeleza kuwa awali walilazimika kukosa huduma za afya wakati wa dharura, huku watoto wakishindwa kufika shule kipindi cha mvua kutokana na hatari ya kuvuka maji. Wamesema hali hiyo sasa imekuwa historia kufuatia uwepo wa daraja hilo.




Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nzali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ametoa ruhusa ya kuanza kutumika kwa daraja hilo licha ya kuwa katika hatua za mwisho za ukamilishaji.


Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kuboresha miundombinu ya usafiri kwa lengo la kuondoa vikwazo vya maendeleo na kuinua maisha ya wananchi, hasa walioko vijijini.


“Mnatakiwa kulitumia daraja hili kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali na biashara ili kujiondoa katika umaskini. Serikali imefanya wajibu wake kwa kujenga miundombinu, sasa ni zamu yenu kunufaika na fursa zinazotokana na uwepo wa daraja hili,” amesema Senyamule





Awali, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, amesema mradi huo mkubwa umegharimu jumla ya Shilingi bilioni 14.5 na unasimamiwa na TANROADS chini ya mkandarasi CHICO.


Amesema daraja hilo limejengwa kwa kuzingatia viwango vya juu vya usalama na uimara ili kudumu kwa muda mrefu, huku akisisitiza kuwa litakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mawasiliano kati ya Kijiji cha Nzali na maeneo mengine ya wilaya ya Chamwino.


Ameongeza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha upatikanaji wa huduma za afya, elimu, masoko ya mazao ya wakulima na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla.


Daraja la Nzali ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ya Serikali inayolenga kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja nchini, hususan katika maeneo ya vijijini, ili kuimarisha ustawi wa wananchi na kuharakisha maendeleo endelevu.






🚨Suscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post