Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeanza mafunzo maalum ya maandalizi ya ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa asali, hatua muhimu inayolenga kuboresha ubora wa taarifa za sekta ya ufugaji nyuki na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa TFS, Hussein Msuya, alisema Tanzania ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa asali duniani, hivyo upatikanaji wa takwimu sahihi ni nguzo muhimu katika kupanga na kuendeleza sekta hiyo.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukitegemea makisio ya Shirika la Chakula Duniani (FAO) yaliyofanywa mwaka 2016, ambayo hayakuwa na uhakika wa kutosha.
Kupitia mafunzo haya tutajikita kupata takwimu halisi za uzalishaji wa asali, mazao mengine ya nyuki, idadi ya wafugaji, mizinga na hata taarifa za mimea inayotoa malighafi ya uzalishaji,” alisema Msuya.
Ameeleza kuwa takwimu hizo zitasaidia kubaini maeneo yenye uzalishaji mkubwa, kufahamu mwelekeo wa sekta na kutambua maeneo yenye fursa kubwa za uwekezaji.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu kutoka Makao Makuu ya TFS, Frida Kundi, alisema mafunzo hayo yamehusisha wataalam kutoka kanda saba za TFS ambao watasambaa katika mikoa mbalimbali kukusanya taarifa hizo muhimu.
“Takwimu hizi ni msingi wa kupanga mipango ya maendeleo ya nchi, kusaidia jamii na kuongeza mchango wa sekta ya nyuki katika uchumi.
Kwa upande wa TFS, taarifa hizi zitatuongoza hata katika kupanga mahitaji ya wataalamu watakaohitajika kuajiriwa,” alisema Kundi.
Naye, mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI), Stanislaus Lukiko, alisema ushirikiano wao na TFS unalenga kuongeza uwezo wa kitaalamu ili kuhakikisha taarifa zitakazokusanywa ni sahihi na zinazoweza kutumika katika kupanga mustakabali wa sekta hiyo.
“Suala la upatikanaji wa takwimu limekuwa changamoto kwa miaka mingi. Tumeungana na TFS kuhakikisha tunapata taarifa za uhakika zitakazosaidia kuendeleza sekta ya ufugaji nyuki,” alisema Lukiko.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuleta mfumo mpya wa ukusanyaji wa takwimu za uzalishaji wa asali nchini, hatua itakayoongeza uwazi, uaminifu na kuchochea maendeleo ya sekta ya nyuki Tanzania.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.




