TEMBO WAVAMIA ILANGALI, WENYEJI WAOMBA SERIKALI KUONGEZA ULINZI.


Na Carlos Claudio, Dodoma.📍


Wakazi wa Kijiji cha Ilangali, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kukabili ongezeko la uvamizi wa tembo wanaoingia kutoka Hifadhi ya Muhezi Kizigo na kusababisha vifo, uharibifu wa mazao na kuongezeka kwa hofu ya baa la njaa.


Wito huo umetolewa wakati wa mazishi ya mtoto aliyefariki dunia baada ya kushambuliwa na tembo kijijini hapo, tukio lililowaacha wananchi katika majonzi na taharuki kubwa.


Wakizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo, baadhi ya wakazi walisema matukio ya tembo kuvamia makazi yao yamekuwa ya mara kwa mara, huku hatua za udhibiti zikidaiwa kuwa ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa tatizo.


“Tunaishi kwa hofu. Tembo wanakuja usiku na mchana, wanaua watu na kula mazao yetu. Tumechoka kufiwa, tumechoka njaa. Tunaomba Serikali ituangalie kwa huruma,” alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho.


Kwa mujibu wa wananchi, mashamba ya mahindi, mtama, uwele na mazao mengine yamekuwa yakiharibiwa mara kwa mara, hali inayodaiwa kuathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa chakula na kipato katika kaya nyingi.


Uongozi wa kijiji wakiri uwepo wa tatizo

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilangali, Bwana Jockitani Mlindwa, alithibitisha kuwepo kwa ongezeko la matukio ya tembo kuingia kijijini, akisema kuwa juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika lakini bado hazijazuia madhara kwa wananchi.


“Hili ni tatizo kubwa. Tembo wanatoka hifadhini na kuingia kwenye maeneo ya wananchi mara kwa mara. Tumejaribu kutoa taarifa mara nyingi, lakini bado changamoto ipo kubwa. Tunaomba msaada wa haraka,” alisema Mlindwa.


Wananchi wataka hatua za haraka ma baadhi ya mapendekezo ya wananchi ni pamoja na kuongezwa kwa doria za askari wanyamapori, kufungwa kwa uzio (fence) kuzunguka maeneo hatarishi, kupewa vifaa vya kujihami kama mizinga ya nyuki na taa maalum zinazowazuia tembo na kulipwa fidia kwa majeruhi, wafiwa na wamiliki wa mazao yaliyoharibiwa.


Wananchi wamesema kuwa bila hatua za haraka, maisha, uchumi na usalama wao utaendelea kuwa mashakani hasa kipindi hiki wanapokabiliwa na tishio la njaa kutokana na uharibifu wa mashamba.







🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post