Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
MKUU wa Wilaya ya Dodoma mjini , Alhaj Jabir shekimweri , amewanyooshea kidole maafisa wa kilimo na mifugo kwa kutokuwapo kwenye Maonesho ya Wahandisi yanayoendelea katika Viwanja vya Nyerere Square, akisema kitendo hicho kinawanyima wananchi fursa muhimu za kupata maarifa ya kisasa.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya Mat Builders & Contractors, Shekimweri alisema uwepo wa maofisa hao ungewezesha wakulima na wafugaji kupata mbinu mpya za teknolojia pamoja na taarifa za upatikanaji wa vifaa vya kazi kwa makubaliano rafiki ya malipo.
“Shekimweri alisema ni wajibu wa maafisa wa kilimo na mifugo kupanga utaratibu wa kuwaleta wakulima na wafugaji kutoka kila kata ili wajifunze. Hizi teknolojia na fursa zilizopo hapa ni msaada mkubwa kwao na kwa uchumi wa Taifa,” alisema.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alibainisha kuwa maonesho hayo yamekuwa kichocheo cha maendeleo na yanaunga mkono jitihada za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan
, hususan katika matumizi ya nishati safi na kuhamasisha wananchi kufanya kazi kwa bidii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mat Builders & Contractors Global Agency, Mhandisi Benard Mwata, alisema lengo kuu la maonesho hayo ni kuandaa wahandisi wenye ujuzi katika sekta za ujenzi na madini.
Aliongeza kuwa taasisi hiyo inashirikiana kwa karibu na ERB pamoja na wizara husika kupromoti elimu ya uhandisi na ukandarasi, huku ikitoa kipaumbele kwa wanawake katika taaluma hizo na kuwaandaa wahandisi chipukizi kupitia programu ya Young Engineer.
Mwata alisema maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza ubunifu, kuongeza uelewa wa kitaaluma na kuunganisha wataalamu na wananchi wanaohitaji huduma za ujenzi na teknolojia mpya.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.





