Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepiga hatua kubwa katika mageuzi ya sekta ya elimu nchini, baada ya kutangaza rasmi kuwa elimu ya lazima sasa itakuwa miaka 10 kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa sawa ya kujifunza, kukuza maarifa na kupata ujuzi utakaomwezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Akizungumza leo, Oktoba 22, 2025, jijini Dodoma katika mkutano wa mwaka wa tathmini ya pamoja ya sekta ya elimu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Prof. Daniel Mushi, alisema kuwa maboresho hayo makubwa yatahitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali, wadau wa elimu na jamii kwa ujumla.
“Mageuzi haya ni ya kimkakati. Tunataka elimu ya lazima iwe jumuishi, yenye ubora na inayomwandaa mwanafunzi kuwa mbunifu na mwenye mchango chanya katika maendeleo ya taifa. Tunatambua ipo haja ya kuongeza miundombinu, walimu na sera shirikishi,” amesema Prof. Mushi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Simon Nanyaro, alisisitiza kuwa wadau wa elimu wako tayari kushirikiana na serikali katika kutekeleza sera hiyo kwa ufanisi.
“Tumejipanga kugema rasilimali na kufanya uwekezaji mkubwa katika elimu. Hili ni jukumu la wote kwa maendeleo ya taifa letu,” alisema Nanyaro.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Lughano Kusiluka, ameeleza kuwa uwekezaji wa serikali katika elimu, hususan kupitia mradi wa HEET, utachochea ubunifu na kuimarisha elimu ya amali nchini.
“Elimu ya amali ni nguzo ya ubunifu. Mradi wa HEET umeleta fursa kubwa za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, jambo litakalowawezesha wanafunzi kuwa wabunifu zaidi,” amesema Prof. Kusiluka.
Mwakilishi wa BASUTA, Bw. Mussa Buluki, amesema taasisi hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada zote zinazolenga kuboresha sekta ya elimu, huku akiwasisitiza wadau wengine kushirikiana katika mabadiliko haya ya kimkakati.
Katika upande wa wanafunzi, Rehema James Mgala, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kisasa, ameshukuru fursa ya kushiriki mkutano huo, akisema elimu ya amali imekuwa na manufaa makubwa katika maisha yao ya kila siku.
“Tunachojifunza hakibaki darasani pekee. Tunatumia elimu ya amali katika miradi midogo midogo ya ubunifu na kujitegemea,” alisema Rehema kwa furaha.
Mkutano huo wa siku tatu umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu kutoka serikalini, taasisi binafsi, vyuo vikuu na mashirika ya maendeleo, ukiwa na kaulimbiu: “Mageuzi ya Elimu kwa Maendeleo Endelevu.”
Kupitia maazimio yatakayofikiwa, serikali inatarajia kuunda mfumo madhubuti wa elimu utakaomjenga kijana wa Kitanzania kuwa mwenye maarifa, ujuzi na maadili bora kwa ustawi wa taifa.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.









