Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
📌Zaidi ya washiriki 2,500 watarajiwa, kampeni yasisitiza uadilifu na ushirikiano wa wananchi.
Mbio maarufu za Sepesha Rushwa Marathon msimu wa nne zimezinduliwa rasmi jijini Dodoma Oktoba 16, 2025, zikiwa na dhamira ya kuhamasisha mapambano dhidi ya rushwa kupitia michezo na kuimarisha umoja wa Watanzania.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma, Eugenius Bernard, alisema mbio hizo ni jukwaa la kipekee la kuunganisha wananchi katika vita dhidi ya rushwa kwa ajili ya maendeleo endelevu ya taifa.
“Kaulimbiu ya mwaka huu ‘Sepesha Rushwa, Kimbia kwa Uadilifu – Run for Integrity’ inatukumbusha kwamba mapambano haya si jukumu la taasisi pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania. Tunakimbia kwa pamoja ili kufikisha ujumbe wa uadilifu na uwajibikaji,” alisema Bernard.
Bernard aliongeza kuwa TAKUKURU mkoa wa Dodoma haiishii kuwa mlinzi wa sheria pekee, bali ni mshirika wa wananchi katika kulinda rasilimali za umma, haki na utu wa kila mmoja. Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya Serikali na wananchi katika kufanikisha vita dhidi ya rushwa.
“Taasisi imeendelea kuhamasisha wananchi kupitia kampeni ya Badili Tabia, Sepesha Rushwa, ambayo imeleta mwamko mkubwa kwa vijana, wanawake, viongozi wa dini na wafanyabiashara kushiriki katika kujenga jamii yenye uadilifu,” aliongeza.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Sauti ya Wapinga Rushwa (SAWARU), Eliasa Abdallah, alisema zaidi ya washiriki 2,500 wanatarajiwa kushiriki katika mbio hizo zitakazofanyika Novemba 30, 2025 katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Abdallah alieleza kuwa mbio hizo zinalenga mambo matatu makuu:
- Kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa
- Kuadhimisha Siku ya Kupinga Rushwa Duniani (Desemba 9)
- Kukusanya fedha za kuendeleza kampeni ya Badili Tabia – Sepesha Rushwa
Kwa mujibu wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na TAKUKURU kwa mwaka wa fedha 2023/2024 zilizowasilishwa Machi 27, 2025, kumekuwepo na mafanikio katika baadhi ya sekta, lakini pia changamoto kadhaa zilibainika, hasa katika usimamizi wa fedha za umma, jambo ambalo taasisi hizo zinasema linahitaji nguvu ya pamoja kulishughulikia.
Uzinduzi wa mbio hizo umepokelewa kwa hamasa kubwa kutoka kwa wakazi wa Dodoma na wadau wa michezo, huku ujumbe ukisisitiza kuwa “kukimbia kwa uadilifu” ni hatua ya kweli ya kulijenga taifa lisilo na rushwa.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.






