MAVUNDE KUWALETEA WANANCHI SULUHISHO LA KUDUMU LA MIGOGORO YA ARDHI

 


Dodoma.📍

Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, amesema anafahamu changamoto ya kutokukamilika kwa zoezi la upimaji wa ardhi kwa wananchi wa eneo la Swaswa Ng’ambo na ameahidi kuwa kabla ya tarehe 15 Novemba, atarudi katika eneo hilo na kurudisha mchakato wa upimaji na umilikishaji ardhi, ili wananchi wapate hati na kuondokana na hofu ya umiliki.


Akiwa katika muendelezo wa kampeni zake  katika Kata ya Ipagala, Mavunde amesema ndani ya miaka mitano ya uongozi wake, wananchi wa Jimbo la Mtumba wataona maajabu ya maendeleo kwani anazijua vizuri kero na changamoto zao kwa kuwa amepita katika mitaa yote, akawasikiliza, na sasa ameziweka moyoni ili azitatue baada ya uchaguzi wa tarehe 29 Oktoba, wananchi watakapomchagua kuwa mbunge wao.


Kuhusu mtaa wa Sulungai, Mavunde amebainisha kuwa changamoto ya migogoro ya ardhi imeanza kushughulikiwa na kazi inaendelea, huku akisema kuwa akichaguliwa, idara ya ardhi itaweka kambi maalum katika kata ya Ipagala ili kuhakikisha wananchi wanamilikishwa ardhi na kupata hati zao.



Aidha, amegusia pia Shule ya Msingi Ilazo, akisema shule hiyo inahitaji nguvu kubwa ya uboreshaji na kwamba yupo tayari kuhakikisha inakamilika. Kwa sasa ujenzi wa matundu ya choo unaendelea, huku Shule ya Msingi Ipagala B ikiwa bado na madarasa machakavu ambayo ameahidi kuyakarabati ili kuhakikisha watoto wanapata mazingira bora ya kujifunzia.


Mavunde amewataka wananchi wa kata ya Ipagala kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 29 Oktoba kuwachagia Mgombea Urais Dkt. Samia S. Hassan,Mgombea Ubunge na Madiwani ili kwa pamoja waweze kuendeleza kazi ya kuwatumikia kwa vitendo na kuhakikisha changamoto zao zinapata suluhisho la kudumu.






🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post