CWT BAHI YAPUUZA BARUA FEKI MTANDAONI, YASISITIZA UTULIVU NA USHIRIKI WA WALIMU KWENYE UCHAGUZI.

 


NA Carlos Claudio, Dodoma.📍


Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Wilaya ya Bahi kimetoa tamko rasmi kikikanusha barua iliyosambaa mitandaoni jana, ikidai kutoa maelekezo kuhusu ushiriki wa walimu katika uchaguzi mkuu ujao.


Akizungumza leo katika wilaya ya Bahi kwa niaba ya Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Bahi, comredy Stephano Mahepe, Katibu wa chama hicho Mwalimu Magreth Mabula amewataka walimu wote wa wilaya hiyo kuipuuza barua hiyo, akibainisha kuwa haijatolewa na uongozi halali wa chama.


“Sisi kama chama cha walimu tuna mfumo rasmi wa mawasiliano unaotoka kwa Katibu Mkuu hadi ngazi za wilaya. Barua yoyote nje ya utaratibu huo si halali,” ameaema Mwalimu Mabula.


Aidha, amewasihi walimu kuendelea kuwa watulivu na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi, akisisitiza umuhimu wa kutimiza haki ya kikatiba bila kuruhusu upotoshaji wa taarifa.


“Ndugu walimu wa wilaya ya Bahi, tuendelee kushiriki katika semina na maandalizi ya uchaguzi kama ilivyopangwa. Tunajivunia utulivu wetu na mwitikio mzuri katika masuala ya kitaifa,” aliongeza.


Mwalimu Mabula pia ameeleza kuwa walimu wengi kwa sasa wapo kwenye semina maalum za uchaguzi, huku wengine wakiendelea kufanya  juhudi za kutoa elimu katika jamii ili wananchi  wajitokeze kwa wingi kupiga kura.


“Tumejipanga kuhakikisha wilaya ya Bahi inakuwa miongoni mwa maeneo yatakayofikia asilimia 100 ya wananchi kujitokeza kupiga kura,” alisema kwa kujiamini.


Amesema Mwenyekiti wa CWT Bahi comredy Stephano Mahepe amehakikisha kwa kusema walimu wa Bahi ni watulivu na watajitokeza kwa wingi kupiga kura.


Akihitimisha taarifa hiyo, Katibu huyo amesisitiza umoja na mshikamano miongoni mwa walimu akisema, Chama cha walimu wilaya ya Bahi kinashirikiana vema na Serikali ,kuhakikisha walimu wanatiza kauli mbiu yetu ya wajibu na haki, “Tuendelee kuchapa kazi, tuwe watulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi. Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki uchaguzi huu uwe salama. Mshikamano daima ndiyo mkombozi wetu.”



🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post