Na Carlos Claudio, Dodoma.📍
Kwa niaba ya washirika wa maendeleo, Bi. Godfrida Magubo, Mkuu wa Ofisi ya Tume ya Uingereza nchini Tanzania, aliipongeza serikali kwa kipaumbele inachokipa elimu chini ya Dira ya 2050, akisisitiza kuwa bila kuwa na wananchi walioelimika vizuri, ukuaji jumuishi hautowezekana.
Akizungumza leo jijini Dodoma katika mkutano wa mwaka wa tathmini ya pamoja ya sekta ya elimu Bi. Magubo ameishauri serikali kuharakisha maandalizi kwa ajili ya mwaka 2027, ambapo takribani wanafunzi milioni 5.1 wataingia katika shule za sekondari za chini kutokana na kupunguzwa kwa muda wa elimu ya msingi kutoka miaka saba hadi sita.
Aidha amesisitiza haja ya kuongeza madarasa, walimu na vifaa vya kujifunzia, na akashauri serikali kushirikiana na sekta binafsi pamoja na taasisi za dini ili kupata rasilimali zaidi.
Serikali imepiga hatua kubwa katika mageuzi ya sekta ya elimu nchini, baada ya kutangaza rasmi kuwa elimu ya lazima sasa itakuwa miaka 10 kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa sawa ya kujifunza, kukuza maarifa na kupata ujuzi utakaomwezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Kupitia maazimio yatakayofikiwa, serikali inatarajia kuunda mfumo madhubuti wa elimu utakaomjenga kijana wa Kitanzania kuwa mwenye maarifa, ujuzi na maadili bora kwa ustawi wa taifa.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.
