MCH. MPONZI AWATAKA WAKRISTO KUWA MAWAKILI WAZURI WA MALI ZA MUNGU

 


Na Carlos Claudio,Dodoma.


Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kaskazini, Mchungaji Erick Mponzi, amewataka Wakristo kuwa mawakili wazuri wa mali za Mungu, akisisitiza kwamba waumini wameaminiwa na Mungu kama wasimamizi imara wa rasilimali zake.



Akizungumza katika Ibada ya Shukrani na uzinduzi wa albamu ya nyimbo za Injili “Bwana Sema Neno” katika Kanisa la Moravian Tanzania, Jimbo Kuu la Kaskazini Ushirika wa Mkonze jijini Dodoma, Mchungaji Mponzi alisema mali alizowapa Mungu wanadamu zinapaswa kugusa maisha ya wengine na kusaidia wenye uhitaji.



Kwa upande wake, Bwana Andrew Mwaipopo, mwandishi mstaafu wa vijana wa Jimbo la Kaskazini na mgeni rasmi wa hafla hiyo, alifafanua maana ya ibada ya shukrani kwa mujibu wa mafundisho ya Kibiblia, akiwahimiza waumini kudumu katika kumshukuru Mungu kwa kila hatua ya maisha yao.


Grace Kamendu, muimbaji na mtunzi wa albamu “Bwana Sema Neno”, alieleza furaha yake kwa kufanikisha kurekodi albamu yake ya pili yenye nyimbo sita na sasa kuzinduliwa rasmi. 



Akiwasilisha risala yake, Grace alisema “Nimefanikiwa kufungua akaunti ya YouTube na matarajio yangu, ndugu mgeni rasmi, ni kwamba baada ya uzinduzi huu tutakusanya kiasi kisichopungua milioni 7, ambacho kitasaidia kufanikisha video ya pili ya muziki wa Injili.”


Grace aliongeza kuwa ana mpango wa kuandika nyimbo nyingi zaidi kadri Roho Mtakatifu atakavyomjalia, akitoa wito kwa waumini na wadau wa Injili kumsaidia kufanikisha huduma hiyo.


Naye Mugabe Mwangoka, Mwenyekiti wa Vijana wa Ushirika wa Iringa Road, alisema tukio hilo limekuwa la baraka kubwa kwa washirika na kutoa wito kwa vijana wenye huduma mbalimbali kanisani kutoacha kutumika kwa Mungu.



“Niwashukuru timu nzima ya maandalizi na Grace kwa moyo wake wa kumtumikia Mungu. Vijana wasikate tamaa, waendelee kufanya kazi ya Mungu kwa bidii,” alisema Mwangoka.


Uzinduzi wa albamu hiyo uliimarisha mshikamano miongoni mwa washirika na kutoa wito wa mshirikiano katika huduma za kijamii, huku viongozi wa kanisa wakisisitiza uwajibikaji na msaada kwa wenye uhitaji kama njia ya kuishi Injili kwa vitendo.












🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.

Previous Post Next Post