ZONGZHOU MINING YAUNGA MKONO SERA YA SERIKALI KUONGEZA THAMANI YA MADINI



Na Carlos Claudio, Dodoma.


Mkurugenzi wa Kampuni ya Zhongzhou Mining Co. Ltd, Bw. Lee Zhong Liang, amemhakikishia Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, kuwa kampuni hiyo itaendelea kudumisha ushirikiano mwema na Serikali pamoja na wananchi wa maeneo yanayozunguka mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha na kusindika madini ya nikeli na shaba, kinachojengwa katika eneo la Zamahero, Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.


Akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo, Bw. Liang alisema Zhongzhou Mining inaunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania kwa kiwango kikubwa.


Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mhe. Mavunde, alisema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi kabla ya kuuzwa nje.


“Ujenzi wa kiwanda hiki ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali kuona Tanzania ikibadilika kutoka wauzaji wa madini ghafi na kuwa taifa linalozalisha bidhaa zenye thamani kubwa kwenye soko la dunia la teknolojia,” alisema Mavunde.


Aidha, Waziri huyo alibainisha kuwa kiwanda hicho chenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 15 kitakapokamilika kitazalisha takribani tani 200,000 za nikeli na shaba kwa mwaka, kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 200 na kuchangia mapato ya Serikali kupitia kodi na tozo mbalimbali.



Mavunde aliongeza kuwa uwekezaji huo ni kielelezo cha utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025 pamoja na Sera ya Madini ya mwaka 2009, inayosisitiza kuongezwa thamani ya madini nchini.


“Kwa sasa Tanzania tunayo viwanda vinane vya kusafisha dhahabu na viwanda tisa vya kuongeza thamani madini ya metali. Mkoa wa Dodoma pekee unajivunia viwanda vitano,” alifafanua Waziri Mavunde.


Naye Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga, alisema uwekezaji wa aina hiyo unaimarisha misingi ya ajira, mapato na ushindani wa uchumi wa Taifa katika soko la kimataifa.


Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bahi, Bi. Mwanamvua Muyongo, alisema kiwanda hicho kitaiweka Wilaya ya Bahi kwenye ramani ya wazalishaji wa bidhaa muhimu za kiteknolojia duniani na kuinua hali ya maisha ya wananchi kupitia ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.













🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya YOUTUBE Ya WASHINDI MEDIA.


🚨FULL VIDEO Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA

Previous Post Next Post