Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewataka wananchi na vikundi vinavyonufaika na mikopo ya asilimia 10 kuhakikisha fedha wanazopata zinatumika ipasavyo na kurejeshwa kwa wakati kama mikataba inavyosema, akisisitiza kuwa mikopo hiyo si zawadi bali ni mikopo nafuu isiyo na riba.
Akizungumza leo katika hafla ya uzinduzi wa Mikopo kwa Mfumo Jumuishi, Mhe. Senyamule amesema serikali imeweka fursa hiyo mahsusi kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, na kuwataka wanufaika kutoona ugumu katika urejeshaji.
“Sitapenda kuona mwanakikundi yeyote anafikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa kushindwa kurejesha mkopo. Ni vyema mkazingatia mkataba mliosaini ili na wengine waweze kunufaika na fedha hizi,” alisema.
Aidha, aliomba benki washirika – CRDB na NMB – kuendelea kutoa elimu kwa vikundi vya wananchi kuhusu masharti na taratibu za mikopo, ili kusaidia kuongeza uelewa na kuepusha changamoto za urejeshaji.
Mkuu huyo wa mkoa alieleza kufurahishwa na mwitikio wa halmashauri katika kuchangia mfuko wa mikopo hiyo, ambapo michango imeongezeka na kufikia Shilingi Bilioni 7.235. Alisema kati ya halmashauri zote nchini, ni chache zenye mapato makubwa zinazoweza kufikia kiwango hicho, na Dodoma Jiji liko miongoni mwao.
“Kwa kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wa mikopo hii, zaidi ya Shilingi Bilioni 6.5 zimetolewa kwa vikundi 546. Huu ni ushahidi wa wazi kuwa jitihada hizi zina mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa wananchi wetu,” alisema Senyamule.
Katika hafla hiyo, jumla ya vikundi 26 vimeanza kunufaika na mikopo yenye thamani ya Shilingi Milioni 313.6, huku vikundi vingine 56 vikisubiri kukamilisha mchakato wa kusaini mikataba ili kukopeshwa Shilingi Milioni 514.5.
Mkuu wa Mkoa alikabidhi hundi kwa benki ya CRDB yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.7 na NMB Shilingi Bilioni 1.9, fedha ambazo zinatarajiwa kufikishwa kwa wanufaika haraka iwezekanavyo.
“Nitoe wito kwa CRDB na NMB kuhakikisha fedha hizi zinawafikia wananchi mapema, kwani wamezisubiri kwa muda mrefu. Serikali yetu imeweka jitihada kubwa kuhakikisha wananchi wanapata mikopo isiyo na riba kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi,” alisisitiza.
Mikopo ya asilimia 10 imekuwa ni sera ya serikali ya Awamu ya Sita katika kuwezesha makundi maalum ya wananchi kiuchumi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
🚨Full VIDEO inapatikana kwenye YouTube Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.






