MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI YATAKIWA KUJENGA UWEZO WA KIFEDHA WA NDANI



Na Carlos Claudio, Dodoma.


Serikali imeyatahadharisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) nchini juu ya mabadiliko ya sera za baadhi ya mataifa wafadhili yaliyosababisha kupungua kwa misaada ya kifedha, na kuyataka kubuni mbinu mbadala za kujipatia rasilimali fedha kupitia vyanzo vya ndani ili kuendeleza huduma kwa Watanzania.


Akizungumza Jumanne, Agosti 12, 2025 jijini Dodoma katika Kongamano la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, alisema hatua hiyo ni muhimu ili kuhakikisha mashirika hayo yanakuwa endelevu katika mazingira ya sasa ya kifedha.


Ni muhimu mashirika haya yasiendelee kutegemea ufadhili wa nje pekee, bali yatafute fursa na mbinu za ndani zinazowezekana ili kuendelea kuhudumia wananchi, alisema Dkt. Jingu.




Kongamano hilo limewaleta pamoja wadau mbalimbali kujadili changamoto na mikakati ya uendelevu, likilenga kuhakikisha huduma kwa jamii zinaendelea kutolewa kwa ufanisi licha ya kupungua kwa misaada kutoka nje.


Dkt. Jingu alibainisha kuwa sheria zinaruhusu mashirika yasiyo ya kiserikali kujihusisha na shughuli za kiuchumi kwa lengo la kujipatia fedha za kujiendeleza, na si kwa kugawana mapato hayo.


Aidha, ameyapongeza mashirika hayo kwa mchango wao katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii, huku akisisitiza haja ya kujenga uwezo wa kifedha wa ndani ili kupunguza utegemezi kwa wadau wa maendeleo na kuimarisha jitihada za kujitegemea.


🚨Subscribe YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA

Previous Post Next Post