Na Carlos Claudio – Dodoma.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ally Hapi, ametoa onyo kali kwa wagombea wa ubunge wa viti maalum kupitia jumuiya hiyo pamoja na wapambe wao, kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi wa chama, huku akiwataka kujiepusha na vitendo vya rushwa na aina yoyote ya mwenendo unaoweza kuathiri uaminifu wao kwa chama.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 31, 2025, jijini Dodoma, Hapi amesema uchaguzi huo muhimu utafanyika kesho Agosti 1, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, ambapo jumla ya wajumbe 756 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanatarajiwa kushiriki.
“Mchakato huu unahitaji uadilifu wa hali ya juu. Tunawaonya wagombea wote na wapambe wao kutojihusisha na vitendo vya rushwa. Chama hakitavumilia na vyombo vya dola vipo macho,” alisema Hapi.
Katibu huyo amesisitiza kuwa ushindani unaotarajiwa kesho ni mkubwa, hivyo wagombea wanapaswa kutegemea sifa zao na si mbinu haramu kupata nafasi.
“Wale ambao hawatapata nafasi kwenye uchaguzi huu, nawasihi waendelee kuwa watulivu na waendelee kuwa waaminifu kwa chama. Siyo kila mmoja atapata nafasi, lakini chama kinathamini mchango wa kila mmoja,” aliongeza.
Katika kuelekea uchaguzi huo, Hapi amesema jumla ya wagombea 60 walichukua fomu, ambapo 33 walitoka Tanzania Bara na 27 kutoka Zanzibar. Kati yao, Kamati Kuu ya CCM iliridhia majina ya wagombea 19 wa ubunge kutoka Bara, wagombea nane wa uwakilishi Zanzibar, na wagombea sita wa ubunge wa viti maalum kwa upande wa Zanzibar.
“Hivyo kesho tunatarajia jumla ya wagombea 33 wataingia katika kinyang’anyiro. Tunatafuta wagombea wawili wa ubunge kutoka Bara, wawili wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, na wawili wa ubunge wa viti maalum Zanzibar,” alisema.
Amesisitiza kuwa Jumuiya ya Wazazi itaendelea kusimamia misingi ya haki, usawa, na uadilifu ndani ya CCM, na kuwataka wajumbe kutumia busara kubwa katika kufanya maamuzi ya kuwachagua viongozi bora.
Mkutano mkuu maalum wa kesho unatarajiwa kuwa wa kihistoria, ukiashiria hatua muhimu katika safari ya chama kuelekea kuimarisha uongozi wake kupitia jumuiya zake.