DODOMA KUWAKA MOTO NA MAADHIMISHO YA SIKU YA HOMA YA INI JULAI 28.



Na Carlos Claudio, Dodoma.


Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini, Dkt. Prosper Njau, ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kupiga hatua katika mapambano dhidi ya homa ya ini huku akisisitiza umuhimu wa jamii kujitokeza kwa wingi kupata elimu, kupima na kupata chanjo ya ugonjwa huo hatari.


Akizungumza leo jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani, Dkt. Njau amesema maadhimisho ya kitaifa mwaka huu yatafanyika tarehe 28 Julai 2025, katika ukumbi wa Morena, jijini Dodoma. Kauli mbiu ya mwaka huu ni: “Ondoa Vikwazo Kutokomeza Homa ya Ini.”


“Tunatumia siku hii kutoa elimu ya kina juu ya namna homa ya ini inavyoambukizwa, athari zake kiafya na hatua za kinga. Homa ya ini aina B haina tiba ya uhakika, lakini kwa bahati nzuri kuna chanjo inayoweza kuzuia,” amesema Dkt. Njau.


Kwa mujibu wa Dkt. Njau, serikali tangu mwaka 2013 ilibadili rasmi mpango wa kudhibiti UKIMWI na kuujumuisha pia magonjwa ya ngono na homa ya ini, kutokana na kufanana kwa njia za maambukizi ya magonjwa hayo.


Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya, Mhe. Jesmista Mhagama.



Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Nelson Bukuru, amesema mkoa huo una furaha kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo, ambapo shughuli mbalimbali za afya zitaanza Julai 26 hadi kilele Julai 28, katika viwanja vya Mashujaa.


“Tunakaribisha wananchi wote kuhudhuria na kufaidika na huduma za bure ikiwemo upimaji wa homa ya ini, UKIMWI, kisukari, shinikizo la damu, chanjo ya homa ya ini pamoja na elimu ya afya kwa ujumla,” amesema Bukuru.



Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Recovery Youth With Vision (REYOVI), Eliaza Ngoda, amesema kuwa maadhimisho hayo ni ya muhimu sana hasa kwa makundi yaliyo hatarini kupata maambukizi, hasa waraibu wa dawa za kulevya.


“Wengi wetu tumepata maambukizi kutokana na kushirikiana sindano. Tunashukuru kwa elimu na chanjo zinazotolewa — zinaokoa maisha,” amesema Ngoda.


Katika siku hizo, pia kutafanyika kampeni ya uchangiaji damu salama, jambo ambalo linatarajiwa kusaidia kuokoa maisha ya maelfu ya watu wanaohitaji damu hospitalini.



💥Full VIDEO Inapatikana Katika YOUTUBE Channel Yetu Ya WASHINDI MEDIA

Previous Post Next Post