Na Carlos Claudio, Dodoma.
Katika maadhimisho ya Siku ya Mtama Kitaifa, wakulima wa kijiji cha Hombolo mkoani Dodoma wameisifu Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwapatia elimu ya matumizi ya mbegu bora za kisasa, hatua iliyoleta mapinduzi makubwa kwenye uzalishaji wa zao la mtama.
Kupitia ushirikiano wa karibu kati ya TBL na maafisa kilimo wa vijiji, wakulima wameweza kupata maarifa ya kisasa yaliyosaidia kuachana na mbegu za kienyeji zisizo na tija na hatimaye kuongeza mavuno na kipato.
Charles Leganda, mmoja wa wakulima kutoka kijiji hicho, amesema kuwa elimu waliyoipata imekuwa chachu ya mabadiliko ya fikra na utendaji.
“Sio tu tumefundishwa kuhusu mbegu bora, bali pia tumejifunza namna ya kuongeza thamani kwenye kilimo chetu. Tunaiona tofauti kubwa kwenye mavuno na maisha yetu kwa ujumla,” amesema Leganda kwa furaha.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa TBL, Bi. Neema Temba, amesema kuwa kampuni hiyo imeamua kushirikiana na wakulima wa ndani kwa dhati kama sehemu ya mkakati wa maendeleo jumuishi.
“TBL inatambua kuwa mazao ya wakulima wa ndani ni sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani wa bidhaa zetu. Tunatamani kuona mkulima anafaidika moja kwa moja kupitia ushirikiano huu,”amesema Neema.
Kwa miaka ya hivi karibuni, TBL imekuwa ikiongeza jitihada za kushirikiana na wakulima katika mikoa mbalimbali ya Tanzania, hasa katika kuhakikisha kwamba kilimo kinabadilika kutoka kilimo cha kujikimu na kuwa kilimo cha biashara.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gelard Mweli, amepongeza mchango wa TBL na kutoa wito kwa makampuni mengine kushirikiana na serikali katika kuimarisha sekta ya kilimo.
“Sekta binafsi ni mhimili muhimu wa maendeleo ya kilimo. Tunahitaji wawekezaji na wazalishaji kuongeza juhudi katika kuwawezesha wakulima wetu kwa kuwapatia mbegu bora, elimu na soko la uhakika,” alisema Katibu Mkuu.
Maadhimisho ya Siku ya Mtama mwaka huu yamekuwa ushahidi tosha kuwa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali unaweza kuleta mapinduzi ya kweli kwa wakulima wa Tanzania. Kupitia TBL, wakulima wa Hombolo si tu wameongeza uzalishaji, bali wamefungua ukurasa mpya wa matumaini katika maisha yao ya kila siku.
🚨Subscribe YouTUBE Channel yetu ya WASHINDI MEDIA.